Sunday, June 02, 2013

ASKARI WAWILI WA NIGER WAUAWA KATIKA JARIBIO LA WAFUNGWA KUTOROKA GEREZANI

Askari wawili wa gereza kuu la Niamey nchini Niger wameuawa baada ya kushambuliwa na wafungwa watatu waliokuwa katika jaribio la kutoroka gerezani hapo siku ya jumamosi. Akizungumza kupitia televisheni ya Taifa ya nchi hiyo, Mwendesha mashtaka Ibrahim Wazir Moussa amewataja wafungwa hao kuwa ni wale wanaotumikia kifungo baada ya kupatikana na makosa ya ugaidi. Askari wengine watatu walijeruhiwa katika mapambano hayo, huku mmoja wao akiwa katika hali mbaya.
Waziri wa Sheria ambaye pia ni msemaji wa serikali ya Niger Marou Amadou ameliambia shirika la habari la AFP wafungwa watatu walidhibitiwa kati ya wanne waliotajwa kuhusika na tukio hilo. Gereza hilo linahifadhi wafungwa zaidi ya 600 wakiwamo baadhi ya wanachama wa kundi la Boko Haram la nchini Nigeria na wengine kutoka vikundi mbalimbali vya wapiganaji wa kiislamu. Uvamizi huo unakuja juma moja tangu kutokea kwa milipuko ya mabomu mei 23 katika kituo cha jeshi cha Agadez ambapo wanajeshi 18 na mwananchi mmoja waliuawa. Makundi mawili ya waislamu wenye msimamo mkali ya Magharibi mwa Afrika MUJAO na Signatories in Blood yamekiri kuhusika na mashambulio hayo yakieleza kuwa hicho ni kisasi kwa Niger ambayo imejiingiza katika mapambano dhidi ya makundi hayo katika nchi jirani ya Mali.

No comments:

Post a Comment

TUPE MAWAZO YAKO