Friday, June 28, 2013

RAIA WAKESHA KUMUOMBEA MANDELA

Raia wa Afrika Kusini wakesha usiku kucha wakimuombea rais wa zamani wa nchi hiyo Nelson Mandela kinara wa zamani nje ya hospitali anakoendelea kupata matibabu mjini Pretoria. Mbali na maombi, raia hao wamekuwa wakiimba nje ya makaazi ya zamani ya kiongozi huyo wa zamani mtaani Soweto. Siku ya Alhamisi rais Jacob Zuma alisema kuwa afya ya Mandela ilionekana kuimarika lakini bado yuko katika hali mbaya.
Binti ya Mandela Makaziwe Mandela amesisitiza  kuwa licha ya baba yake kuwa katika hali mbaya, bado wana imani atapata nafuu na kuondoka hospitalini. Hata hivyo, Makaziwe amevishtumu vyombo vya habari vya kimataifa kuwapotosha watu duniani na halikadhalika kutoipa familia nafasi ya kuwa binafsi. Mbali na hayo rais wa Marekani Barrack Obama anatarajiwa kuwasili nchini humo hivi leo akitokea nchini Senegal ambako yupo kwenye ziara barani Afrika.
Jana rais Obama alikutana na Majaji wakuu wa Mahakama za juu barani Afrika jijini Dakar nchini Senegal na kujadiliana kuhusu haki barani Afrika. Aidha, Obama aliisifu nchi ya Senegal kama mojawapo ya nchi barani Afrika inayoimarika kidemokrasia na kufanya mabadiliko katika taasisi zake. Obama anatarajiwa kukutana na rais wa Afrika Kusini Jacob Zuma pamoja na wafanyibiashara na viongozi wa vijana wakati huu rais wa kwanza mweusi wa taifa hilo Nelson Mandela akiendelea kupata matibabu hospitalini. Baada ya kuondoka Afrika Kusini Obama anatarajiwa kuzuru Tanzania siku ya Jumatatau juma lijalo.

No comments:

Post a Comment

TUPE MAWAZO YAKO