Wednesday, June 26, 2013

RAIS WA UFARANSA AAHIDI KUPAMBANA NA CHUKI DHIDI YA UISLAM

Rais Francois Hollande wa Ufaransa ameahidi kupambana na wimbi la uadui na chuki dhidi ya Uislamu katika nchi hiyo ya barani Ulaya. Rais Hollande amesema hayo mbele ya hadhara kubwa ya wawakilishi wa taasisi na asasi za kiserikali na kiraia pambizoni mwa mji mkuu Paris na kusisitiza kwamba, atapambana na wimbi la chuki dhidi ya Uislamu. Hollande anatoa ahadi hiyo katika hali ambayo, katika majuma ya hivi karibuni Waislamu wa Ufaransa hususan wanawake wanaovaa vazi tukufu la hijabu wamekabiliwa na wimbi kubwa la mashambulio ya watu waliofurutu ada na wenye chuki kubwa dhidi ya Uislamu. Miongoni mwa matukio ya chuki dhidi ya Uislamu nchini Ufaransa katika mwaka huu wa 2013 ni kushambuliwa wanawake kadhaa waliokuwa wamevaa hijabu katika kitongoji cha Val-d'Oise kaskazini mwa nchi hiyo. Viongozi wa Muungano wa Taasisi za Kiislamu nchini Ufaransa (UOIF) sanjari na kuonesha wasi wasi wao mkubwa kuhusiana na vitendo hivi ambavyo vimegeuka na kuwa jambo la kawaida, wamewataka viongozi wa serikali kuvunja kimya chao na kuchukua hatua kali za kuhitimisha vitendo hivyo vya kinyama dhidi ya Waislamu. Takwimu zinaonesha kuwa, vitendo vya mashambulio dhidi ya maeneo ya kidini ya Waislamu nchini Ufaransa vimeongezeka mno katika majuma ya hivi karibuni. Baraza la Kiutamaduni la Waislamu nchini Ufaransa (CFCM) limetangaza katika ripoti yake ya hivi karibuni kwamba, tangu kuanza mwaka huu wa 2013 zaidi ya misikiti 10 imeshambuliwa na kuvunjiwa heshima nchini humo. Nayo Kamati ya Kupambana na Kampeni za Kuuogopesha Uislamu nchini Ufaransa (CCIF) imetangaza kuwa, itafuatilia suala la kushambuliwa wanawake wa Kiislamu nchini humo. Katika hali ambayo vyombo vya habari vya Ufaransa vinafumbia macho mashambulio dhidi ya wanawake wa Kiislamu nchini humo, hivi karibuni wanawake wanne wa Kiislamu walishambuliwa na kupigwa vibaya katika viunga vya Paris. Mmoja wa wanawake wa Kiislamu ambaye alishambuliwa katika mji wa Argenteui aliumia vibaya na kusababaisha mimba yake kutoka.  Wataalamu wa mambo wanaamini kwamba, makundi yenye kufurutu ada na yenye chuki na Uislamu yameingiwa na wasi wasi na kihoro kikubwa kutokana na kuongezeka kwa kasi idadi ya Waislamu barani Ulaya hususan nchini Ufaransa. Hivi sasa malalamiko makubwa ya Waislamu wa Ufaransa ni hatua ya vyombo vya habari vya nchi hiyo ya kunyamazia kimya mashambulio na vitendo vya ubaguzi dhidi ya Waislamu. Ufaransa ina wakazi milioni 62.3 huku milioni 6 wakiwa ni Waislamu. Wataalamu wa mambo wanasema kuwa, Ufaransa inashikilia nafasi ya kwanza barani Ulaya kwa kuwa na idadi kubwa ya Waislamu na dini ya Kiislamu inahesabiwa kuwa ya pili kwa ukubwa nchini humo baada ya Ukristo. Hivyo basi kuongezeka vitendo vya chuki na mashambulio dhidi ya Waislamu vinaweza kutathminiwa katika fremu ya hofu na wasi wasi wa kupata nguvu Uislamu nchini Ufaransa.

No comments:

Post a Comment

TUPE MAWAZO YAKO