Friday, July 12, 2013

ETHIOPIA YALAANI MAUAJI YA WANAZUONI

Wizara ya Mambo ya Nchi za Nje ya Ethiopia na chama tawala nchini humo, kwa pamoja zimetoa taarifa za kulaani kitendo cha kuuawa mwanachuoni mashuhuri wa Kiislamu nchini humo. Wizara ya Mambo ya Nchi za Nje ya Ethiopia imetoa taarifa ya kulaani vikali kitendo cha kuuawa Sheikh Nuru Yimam, mmoja wa maulamaa mashuhuri katika jimbo la Amhara kaskazini mwa nchi hiyo. Wakati huohuo, chama tawala cha Ethiopian People's Revelutionary Democratic Front (EPRDF) kimelaani kitendo cha kuuawa Sheikh Nuru Yimam na kuwataka wananchi wa Ethiopia kushirikiana na serikali kwenye mapambano dhidi ya vitendo vya kigaidi.
Taarifa kutoka Addis Ababa zinasema kuwa, jeshi la polisi nchini humo tayari limeshawatia mbaroni watuhumiwa kadhaa wa shambulio hilo la kigaidi. Inafaa kuashiria hapa kuwa, Sheikh Nuru Yimam aliuawa kwa kupigwa risasi kadhaa siku ya Jumanne iliyopita katika mji wa Amhara kaskazini mwa Ethiopia wakati alipokuwa akitoka Msikitini. Maelfu ya Waislamu nchini Ethiopia wamefanya maandamano wakitaka kutiwa mbaroni na kufunguliwa mashtaka wahusika wote wa kitendo hicho cha kinyama.

No comments:

Post a Comment

TUPE MAWAZO YAKO