Wednesday, July 24, 2013

GHASIA ZAIBUKA BRAZIL KATIKA MAPOKEZI YA PAPA

Kiongozi wa Kanisa Katoliki Duniani Papa Francis amepokelewa kwa shangwe nchini Brazil ikiwa ni ziara yake ya kwanza rasmi ya nje tangu apate nafasi hiyo na ameianza katika nchi ambayo inatajwa kuwa na waumini wengi zaidi wa kanisa hilo Duniani. Papa Francis amepata mapokezi hayo ya kipekee licha ya kwamba katika baadhi ya maeneo kumekuwa na maandamano yaliyoambatana na ghasia kupinga ujio wake nchini Brazil kitu kilichowapa wakati mgumu askari. Jeshi nchini Brazil lilikuwa na kibarua kigumu kukabiliana na waandamanaji hao ambao wanakosoa kufanyika kwa ziara hiyo ya Papa Francis nchini humo wakidai nchi hiyo imeshindwa kusikiliza matakwa ya wananchi wake.
Waandamanaji hao wakiwa wamebeba bendera za taifa la Brazil pamoja na kuimba nyimbo mbalimbali wamejitokeza kwenye mitaa ya Jiji la Rio De Janeiro kitu kilichochangia Jeshi kutumia mabomu ya machozi na maji ya kuwasha kuwatawanya. Waandamanaji hao walikuwa wanashinikiza kusikilizwa ili watume ujumbe wao kwa Papa Francis alipokuwa anakutana na Rais Dilma Rousseff ambaye akikabiliwa na maandamano ya kukosoa sera zake katika kuboresha maisha ya wananchi. Wananchi hao waliojitokeza mitaani wameendelea kushinikiza Rais Rousseff kuondoka madarakani kutokana na kushindwa kuboresha maisha ya wananchi wake tangi aingie madarakani kitu kilichochangia hali ngumu ya maisha. Licha ya uwepo wa maandamano na ukosoaji dhidi ya ziara hiyo ya juma moja ya Kiongozi wa Kanisa Katoliki Duniani nchini Brazil Papa Francis kuna wale ambao walijitokeza na kufurahia ujio wake.
Wengi waliojitokeza kumpokea Papa Francis wamesema hii ni ziara ya kipekee ambayo itasaidia kuimarisha uhusiano wa waumini wa Kanisa Katoliki Duniani hasa ukitilia maanani nchi hiyo ndiyo inawaumini wengi zaidi. Ziara ya Papa Francis nchini Brazil itamchukua kipindi cha juma moja na inatajwa huenda ikawa ni ziara ndefu zaidi ya nje ya Vatican kufanywa na Kiongozi huyo ambaye amekuwa akisisitiza umoja wa waumini wa kanisa hilo

No comments:

Post a Comment

TUPE MAWAZO YAKO