Wednesday, July 24, 2013

WATU TISA WAFARIKI KATIKA GHASIA MPYA ZA MISRI

Watu tisa wamepoteza maisha nchini Misri na wengine ishirini na wanane wakijeruhiwa baada ya kuzuka makabiliano makali baina ya wafuasi wa Mohamed Morsi aliyeondolewa madarakani na Jeshi dhidi ya wale wanaompinga kipindi hiki familia yake ikijiandaa kumshtaki Mkuu wa Majeshi Jenerali Abdel Fattah Al Sisi. Mapambano makali yalishuhudiwa katika Mji wa Qalyub wakati ambapo maandamano yaliendelea kushuhudiwa katika Jiji la Cairo kitu kilichochangia Jeshi kuingilia kati kwa ajili ya kurejesha hali ya utulivu wa maeneo hayo. Wafuasi wanaomuunga mkono Morsi ambaye bado anashikilia na Jeshi wamejiapiza kuendelea kufanya maandamano yao kwenye Miji mbalimbali wakiwa na lengo la kushinikiza kurejeshwa madarakani kwa Kiongozi huyo aliyeondolewa na Jeshi.
Ghasia hizo zilishuhudiwa hata katika Wilaya ya Sinai iliyopo Kaskazini mwa Taifa hilo ambapo raia mmoja alipoteza maisha na wanajeshi wanne wamejeruhiwa baada ya kutokea shambulizi lililowalenga. Rais wa Mpito wa Misri Adly Mahmud Mansour ameendelea kutoa wito kwa pande zinazohasimiana kuhakikisha hali ya utulivu inarejea nchini humo ili wananchi washiriki kwenye ujenzi wa taifa kipindi hiki akitaja kikosi ambacho kitakuwa na jukumu la kupitia katiba na kupendekeza mabadiliko. Haya yanakuja baada ya familia ya Morsi kupitia Mtoto wake wa Kike Shaimaa Mohamed Morsi kutangaza nia yao yakumfungulia mashtaka Mkuu wa Majeshi Jenerali Al Sisi kutokana na kuendelea kumshikilia Kiongozi huyo wa zamani.
Shaimaa amewaambia wanahabari watafungua mashtaka hayo kwa kuzingatia sheria za ndani na hata zile za kimataifa kwa kuwa wanaona kinachoendelea kufanywa na Jeshi chini ya Jenerali Al Sisi ni utekeji nyara. Familia ya Morsi imeweka bayana imechoshwa na hatua ya kuendelea kusubiri kuachiwa kwa Kiongozi huyo wa Chama Cha Muslim Brotherhood aliyechanguliwa kwa njia ya kidemokrasia na kukaa madarakani kwa kipindi cha mwaka mmoja pekee. Mohamed Morsi aliondolewa madarakani tarehe 3 ya mwezi Julai kutokana na kutuhumiwa na maelfu ya wananchi amekuwa akipendelea wafuasi wa Chama Cha Muslim Brotherhood na hivyo maandamano yakaanza kwenye viunga vya Tahrir kushinikiza aondoke madarakani.
Jeshi nchini Misri likaamua kuingilia kati mgogoro huo wa kisiasa na kumtaka Morsi kuzungumza na pande zote kusaka suluhu ya kisiasa kitu ambacho alikikaidi hivyo Jeshi likamuondoa madarakani na kumshikilia sehemu ambayo haijulikani hadi sasa.

No comments:

Post a Comment

TUPE MAWAZO YAKO