Tuesday, July 02, 2013

ZIMBABWE NJIA PANDA

Waziri wa Sheria na Masuala ya Bunge wa Zimbabwe Patrick Chinamasa ametangaza kuwa baada ya kuvunjwa bunge la nchi hiyo Rais Robert Mugabe ndiye atakayekuwa marejeo pekee ya utungaji sheria.
Duru ya miaka mitano ya kuweko madarakani kisheria bunge la Zimbabwe ilimalizika Juni 29 mwaka huu na kwa mujibu wa katiba ya nchi hiyo majukumu ya bunge yatakuwa chini ya Rais hadi utakapofanyika uchaguzi mpya wa bunge. Hii ni katika hali ambayo, licha ya majadiliano na mashauriano mengi ya viongozi wa vyama vinavyohasimiana huko Zimbabwe, lakini tarehe ya kufanyika uchaguzi huo mpya bado haijaainishwa.
Robert Mugabe kiongozi wa chama cha Zanu-PF ametangaza siku ya tarehe 31 Julai kuwa ni siku inayofaa kwa ajili ya kufanyika uchaguzi. Hata hivyo wapatanishi wa Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC) wanasisitiza kwamba uchaguzi unapasa kuakhirishwa kwa muda wa wiki mbili.
Naye Waziri Mkuu wa Zimbabwe Morgan Tsvangirai anaona kuwa kipindi hicho cha wiki mbili hakitoshi kwa ajili ya kutekelezwa marekebisho ya kimsingi nchini humo. Uchaguzi wa Rais na Bunge jipya la Zimbabwe unatazamia kuhitimisha shughuli za serikali ya mseto na umoja wa kitaifa. Weledi wa masuala ya kisiasa wanaamini kuwa mashinikizo yanayotolewa na Mugabe na wafuasi wenye kufurutu ada wa chama chake cha Zanu-PF kwa ajili ya kufanyika uchaguzi haraka huko Zimbabwe yana lengo la kuhitimisha kazi na utendaji wa serikali ya mseto.
Chama tawala zamani ya cha Zanu-PF kinachoongozwa na Mugabe mwezi Septemba mwaka 2008 kililazimika kwa mara ya kwanza kusaini makubaliano ya kugawana madaraka na wapinzani kufuatia mashinikizo ya kisiasa ya viongozi wa jumuiya ya SADC. Hatimaye serikali ya mseto  iliundwa huko Zimbabwe mwezi Februari mwaka uliofuata kwa kuvishirikisha vyama vitatu vikubwa yaani Zanu-PF, MDC na kile kilichoasisiwa kutokana na tawi lililojitenga na chama hicho cha upinzani. Vipengee vya katiba ya Zimbabwe vinabainisha wazi kuwa uchaguzi mpya unapasa kufanyika miezi 18 baada ya kuundwa serikali ya mpito.  Hata hivyo hitilafu za kimitazamo kati ya vyama vinavyounda serikali zinazuia kufanyika uchaguzi huo.
Katika muda wote huo ambapo Zimbabwe imekuwa ikikabiliwa na hali ya mgogoro, uungaji mkono wa wakuu wa nchi jirani katika jumuiya ya SADC hususan Afrika Kusini umeipa nguvu serikali ya Zimbabwe katika kuamiliana na mashinikizo na vikwazo vya nchi za Magharibi. Aidha hatua ya wafuasi wenye misimamo ya kufurutu ada wa chama Zanu-PF ya kuvuruga mazungumzo kuhusu katiba ya nchi hiyo na kuzusha ghasia dhidi ya wafuasi wa chama cha Mabadiliko ya Kidemokrasia (MDC) imewatatiza viongozi wa SADC. Rais Jacob Zuma wa Afrika Kusini ambaye ni mpatanishi kati mgogoro wa Zimbabwe, alimtishia wazi Mugabe katika vikao vya wakuu wa Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika SADC kuwa anapasa kutekeleza marebebisho ya kisiasa nchini mwake.

No comments:

Post a Comment

TUPE MAWAZO YAKO