Friday, August 09, 2013

AMNESTY YAITAKA ETHIOPIA KUTOWAKANDAMIZA WAISLAM

Shirika la Msamaha Duniani la Amnesty International limeitaka serikali ya Ethiopia iache kuwakandamiza Waislamu wa nchi hiyo. Taarifa ya Amnesty International iliyotolewa hapo jana imeitaka serikali ya Ethiopia iache vitendo vya kuwakandamiza Waislamu. Aidha taarifa hiyo imesema, serikali ya Ethiopia inapaswa kukomesha vitendo vya kukandamiza maandamano ya amani ya Waislamu wa nchi hiyo. Maandamano karibu yote yaliyofanywa na Waislamu wa Ethiopia katika kipindi cha mwaka mmoja na nusu yalikuwa ya amani lakini vikosi vya usalama vya nchi hiyo vilitumia mkono wa chuma kuzima baadhi ya maandamano hayo, imebainisha taarifa ya Shirika la Msamaha Duniani la Amnesty International. Taarifa ya Amnesty International imekuja masaa machache tu baada ya Waislamu wa Ethiopia kuandamana jana baada ya Sala ya Eid ul Fitri wakipinga hatua ya serikali ya kuingilia mambo yao. Kwa siku kadhaa sasa mji mkuu wa Ethiopia Addis Ababa umekuwa ukishuhudia maandamano makubwa ya Waislamu wakilalamikia kitendo cha kuuawa Sheikh Nuru Yimam Muhammad aliyepigwa risasi wakati akitoka msikitini katika jimbo la Amhara, nchini humo. Sheikh Nuru Yimam alikuwa mmoja wa wanaharakati wakubwa wa Kiislamu nchini Ethiopia.

No comments:

Post a Comment

TUPE MAWAZO YAKO