Friday, August 09, 2013

DOLA ELFU 6 KWA ATAYESAIDIA KUKAMATWA WALIOWAMWAGIA TINDIKALI WATALII

Polisi visiwani Zanzibar nchini Tanzania wametangaza donge nono la dola elfu 6170 sawa na paundi za Uingereza elfu 3971 kwa mtu yeyote atakayefanikisha kukamatwa kwa watu wanaodaiwa kuwamwagia tindi kali raia wawili wa Uingereza. Hapo jana jeshi la Polisi lilitangaza kuanza msako mkali visiwani humo kuwasaka watuhumiwa tukio hilo ambapo tangazo la donge nono linakuja wakati ambapo rais wa Jamuhuru Jakaya Kikwete akitaka waliohusika kusakwa popote walipo. Hapo jana rais Jakaya Kikwete aliwatembelea rais hao, Kirstie Trup na Katie Gee ambao walikuwa wamelazwa kwenye hospitali ya Aga Khan jijini Dar es Salaam ambako walisafirishwa kutokea Zanzibar.
Akizungumza na wanahabari muda mfupi baada ya kuwaona wasichana hao, rais Kikwete alisema tukio hilo limechafua sifa ya nchi ya Tanzania na kuliita ni laaibu kwakuwa ni nadra sana kwa wananchi wa Tanzania kutekeleza vitendo kama hivi. Kwa mujibu wa taarofa iliyotolewa na familia ya wasichana hao, imesema kuwa inalaani shambulio hilo baya kutekelezwa dhidi ya watoto wao ambao hawakuwa na hatia na kuwashukuru wanahabari na Serikali kwa ushirikiano waliouonesha. Wote wawili wamesafirishwa kwenda nchini Uingereza usiku wa jana kwa matibabu zaidi.
Kwa mujibu wa taarifa ya jeshi la Polisi, imesema kuwa wasichana hao wanaodaiwa kuwa na umri wa miaka 18 walimwagiwa tindi kali na watu wawili waliokuwa kwenye pikipiki kwenye mji Mkongwe wa Zanzibar na kisha watu hao kutokomea kusikojulikana. Polisi wanasema mpaka sasa hawajabaini sababu za watu hao kutekeleza shambulio hili dhidi ya raia wa kigeni na kwamba uchunguzi unaendelea na kutoa wito kwa wananchi kushirikiana na jeshi hilo kusaidia kuwakamata watu hao.

No comments:

Post a Comment

TUPE MAWAZO YAKO