Friday, August 09, 2013

WAFUASI WA MURSI WAAPA KUTOTAWANYIKA MAENEO WALIYOPO

Wafuasi wa kiongozi aliyeondolewa madarakani nchini Misri, Mohamed Morsi wamesherekea sikukuu ya Eid al-Fitr wakiwa kwenye maeneo wanayoyakalia huku wakiapa kutoondoka licha ya tangazo la Serikali. Usiku wa kuamkia leo maelfu ya wafuasi wa Muslim Brotherhood walionekana kusherekea kwenye viwanja vya mjini Cairo jirani na chuo kikuu cha Cairo wakiimba nyimbo za kukashifu utawala wa kijeshi. Hapo jana mara baada ya sala, wafuasi wa Morsi waliokuwa kwenye uwanja wa Rabaa al-Adawiya walisikika wakiapa kuendelea kusalia kwenye viwanja hivyo licha ya tangazo la Serikali linalowataka kuondoka kwenye maeneo hayo.
Hofu ya kiusalama imeendelea kutanda nchini Misri huku mataifa ya magharibi yakieleza hofu yao kuhusu kuendelea kwa mvutano wa kisiasa kati ya wafuasi wa Morsi na wale wanaounga mkono Serikali ya mpito. Nchi ya Iran imeeleza hofu ya kuzuka kwa vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini humo kutokana na kuendelea kushuhudiwa kwa maandamano kati ya wafuasi wanaomuunga mkono rais Morsi na wale wanaiunga mkono Serikali.

No comments:

Post a Comment

TUPE MAWAZO YAKO