Saturday, August 17, 2013

WAFUASI WA MORSI WAZIDI KUUAWA MISRI

Takriban Wafuasi watano wa Rais wa Misri aliyeondolewa madarakani Mohamed Morsi na Askari mmoja wa kikosi wa usalam wameuawa hii leo baada ya kutokea mapigano katika miji kadhaa kati ya Waandamanaji na Vikosi vya usalama. Watano waliuawa katika mji wa Ismailiya, huku askari mmoja akiuawa baada ya kituo cha ukaguzi alichokuwamo kuvamiwa na Watu wenye silaha jijini Cairo. Ghasia hizo zilijitokeza wakati Waandamanaji walipoanza maandamano katika miji kadhaa maandamano waliyoyaita Ijumaa ya Ghadhabu. 
 Wafuasi wa Chama cha kiislamu cha Muslim Brotherhood waliitisha maandamano siku ya leo kudhihirisha ghadhabu zao baada ya kuuawa kwa Watu takriban 600 wakati vikosi vya usalama vilipokuwa vikisambaratisha makambi yaliyowekwa na Wafuasi wa aliyekuwa Rais wa nchi hiyo, Mohamed Morsi. Wito huu uliongeza hofu ya kuzuka kwa machafuko baada ya yale ya siku ya jumatano hali iliyosababisha Umoja wa Mataifa kukemea Machafuko hayo na kutaka kusitishwa mara moja na pande zote mbili. Hali ya hatari ilitangazwa katika majimbo mengi ya nchini Misri huku kukiripotiwa kuuawa kwa Wanajeshi saba na Askari mmoja kuuawa katika mji wa Assiut. Wizara ya mambo ya ndani ilitoa amri kwa Askari kutumia risasi iwapo majengo ya Serikali yatashambuliwa. Baraza la usalama la umoja wa Mataifa limekemea yanayojiri nchini Misri na kuitisha mkutano wa dharura juu ya Misri, hatua iliyoombwa na Ufaransa, Uingereza na Australia.
 Msemaji wa makundi ya kiislamu yanayomuunga mkono Morsi, Laila Moussa amesema kuwa yamepangwa maandamano nchi nzima hii leo na kuongeza kuwa wafuasi wa Morsi wakiwemo Wabunge wa zamani wamekamatwa wakati wa maandamano . Jijini NewYork Balozi wa Agentina ndanu ya Umoja wa Mataifa, Maria Cristina Perceval, amesema kuwa Wanachama wa Baraza la usalama la umoja wa Mataifa wanasikitishwa na namna ambavyo Wamisri wamekuwa wakipoteza maisha jijini Cairo na kutoa wito wa kufanyika maridhiano ya kitaifa. Jijini Washington, Rais wa Marekani, Barack Obama amesitisha mazoezi ya pamoja ya kijeshi kati ya Marekani na Misri kutokana na yanayojiri hivi sasa nchini Misri. Halikadhalika Wizara ya mambo ya nje ya Marekani imetoa wito kwa Raia wake kutosafiri kwenda Misri na kuwataka Wamarekani walio nchini Misri, kuondoka.

No comments:

Post a Comment

TUPE MAWAZO YAKO