Wednesday, January 16, 2013

ASKARI WA UFARANSA WAANZA OPERESHENI ZA NCHI KAVU


Askari wa Ufaransa walioko nchini Mali wameanza mashambulizi ya nchi kavu dhidi ya waasi wa nchi hiyo. Askari hao waliopelekwa nchini Mali kutokea Chad, Ivory Coast na Gabon kwa siku 5 mtawalia wamekuwa wakifanya mashambulizi ya anga dhidi ya waasi wanaoipinga serikali ya Bamako. Rais Francois Hollande wa Ufaransa amesema kuwa, idadi ya askari wa nchi yake imeongezwa nchini Mali na kufikia 2,500.
Serikali ya Paris imepeleka jeshi nchini Mali kwa kisingizio cha kuzuia kusonga mbele waasi kuelekea maeneo ya kusini mwa nchi hiyo. Hollande anafanya jitihada za kuhalalisha mashambulizi yake ya kijeshi nchini Mali na kupata uungaji mkono wa jamii ya kimataifa kupitia azimio nambari 2058 la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa. Anadai kuwa, mashambulizi ya jeshi na ndege za kivita za Ufaransa nchini Mali yanafanywa kwa mujibu wa sheria za kimataifa. Hata hivyo amesahau kuwa azimio la Baraza la Usalama lililopasishwa Disemba mwaka jana kuhusu mgogoro wa Mali, lilikubali kutumwa askari 3,300 wa kikosi cha Ecomog kaskazini mwa Mali. Kikosi cha Ecomog ni cha nchi wanachama wa jumuiya ya kieneo ya Ecowas, ambayo tangu mwezi Novemba mwaka uliopita ilitangaza kuwa iko tayari kupeleka vikosi vyake huko Mali. Azimio la pili la Baraza la Usalama liliruhusu operesheni za kijeshi za kimataifa nchini Mali chini ya uongozi wa nchi za Kiafrika, na wakati huo huo limesisitiza juu ya kuhitimishwa mgogoro huo kwa njia za kidiplomasia. Hata hivyo azimio hilo halikuanisha muda wa kuanza operesheni za kijeshi za askari wa Kiafrika nchini Mali.
Zaidi ya hayo wajumbe wa Baraza la Usalama walitaka kukarabatiwa jeshi la Mali na kuimarishwa taasisi za ulinzi za nchi hiyo zilizosambaratika baada ya mapinduzi ya kijeshi ya Machi 22 mwaka uliopita. Kwa msingi huo, kusonga mbele waasi kusini mwa Mali na kuelekea mji mkuu, Bamako, kulivipa vikosi vya Ufaransa kisingizio kizuri cha kufanya mashambulizo ya ghafla nchini humo Ijumaa Januari 11. Hofu ya uwezekano wa kudhibitiwa mji mkuu wa Mali na kuanguka mikononi mwa waasi wanaopinga satua na ushawishi wa Ufaransa magharibi mwa Afrika, imetumiwa na Paris kama kisingizio cha kuanza mashambulizi ya ghafla huko Mali. Hii ni katika hali ambayo, kwa mujibu wa azimio nambari 2058 la Baraza la Usalama, operesheni za kijeshi za kukomboa eneo la kaskazini mwa Mali zilipaswa kufanywa na vikosi vya kimataifa kwa kuongozwa na nchi za Kiafrika.
Kwa sasa swali muhimu linaloulizwa ni kuwa, askari wa jumuiya ya Ecowas watapelekwe lini nchini Mali ili kusaidia jeshi la nchi hiyo kukomboa eneo la kaskazini? Inasemekana kuwa askari wa Burkina Faso, Ghana, Nigeria, Niger, Benin, Senegal na Togo wataelekea Mali katika siku chache zijazo.
Marekani na Uingereza zinatoa misaada ya kilojistiki kwa Ufaransa katika mashambulizi  yake ya kijeshi nchini Mali, lakini Russia na China zimeendelea kusisitiza kuwa, mashambulizi yoyote ya kijeshi nchini Mali yanapaswa  kupasishwa na Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa na Umoja wa Afrika (AU). Katika miaka ya hivi karibuni viongozi wa AU pia wamekuwa wakifanya jitihada za kutatua migogoro ya nchi za bara hilo kwa njia zinazobuniwa na nchi za Kiafrika na kupunguza utegemezi wa taasisi na nchi za Magharibi.

No comments:

Post a Comment

TUPE MAWAZO YAKO