Wednesday, January 16, 2013

UJERUMANI NAO KUPELEKA NDEGE MALI

Ujerumani imeahidi kupeleka ndege mbili kwa ajili ya wanajeshi wanaopigana na waasi wenye itikadi kali za Kiislamu kaskazini mwa Mali. Ahadi hiyo imetolewa leo wakati Kansela Angela Merkel alipokutana mjini Berlin na mwenyekiti wa sasa wa Jumuiya ya Kiuchumi ya nchi za Afrika Magharibi-ECOWAS, Alassane Ouattara, ambaye pia ni rais wa Cote d'Ivoire. ECOWAS inajiandaa kupeleka wanajeshi 3,300 nchini Mali ili kuyasaidia majeshi ya nchi hiyo na yale ya Ufaransa kupambana na waasi hao. Ujerumani imesisitiza kuwa haitopeleka wanajeshi, lakini Waziri wake wa Ulinzi, Thomas de Maiziere, amesema nchi yake iko tayari kupeleka ndege mbili zitakazokisaidia kikosi cha ECOWAS. Rais Ouattara anatarajiwa pia kukutana na Waziri wa Mambo ya Nje wa Ujerumani, Guido Westerwelle. Ziara hiyo ilipangwa kabla hali ya Mali haijapamba moto wiki iliyopita kutokana na waasi kusonga mbele kuelekea kusini mwa mji mkuu, Bamako na kuanza kwa operesheni za Ufaransa. Jana wakuu wa kijeshi wa ECOWAS walikutana mjini Bamako kujadiliana kuhusu kikosi hicho. Nigeria, Cote d'Ivoire, Benin, Ghana, Senegal, Niger, Guinea, Burkina Faso na Togo, zimeahidi kupeleka wanajeshi wake.

No comments:

Post a Comment

TUPE MAWAZO YAKO