Monday, March 11, 2013

KUNDI LA ANSARU LASEMA LIMEWAUWA MATEKA SABA WAKIGENI


Madai ya kundi moja la wapiganaji wa kiisilamu nchini Nigeria, kuwa limewaua mateka saba wa kigeni waliowateka nyara mwezi jana huenda ni ya kweli, kulingana na duru za kigeni. Mateka hao kutoka nchini Italy, Uingereza, Ugiriki, na Lebanon, walitekwa katika eneo la mjengo katika jimbo la Bauchi Kaskazini mwa nchi. Katika taarifa iliyopeperushwa kupitia kwa mtandao, siku ya Jumamosi,kundi la wapiganaji la Ansaru lilidai kuwaua mateka hao. Ansaru linashukiwa kuwa kundi lenye kuendesha harakati sawa na za Boko Haram.
Jumapili, waziri wa mambo ya nje wa Uingereza William Hague, alisema kuwa mfanyakazi wa mjengo aliyetajwa kama Brendan Vaughan, huenda aliuawa na watu waliokuwa wamemteka, pamoja na wenzake sita. "haya ni mauaji mabaya sana ambayo, hayana sababu hata moja , na haifai kwa kitendo kama hiki kutendwa,'' aliongeza bwana Hague. Serikali ya Italia iliwasilisha taarifa sawa na hiyo wakati wizara ya mambo ya nje ya Ugiriki ikisema , kuwa taarifa waliyonayo inaonyesha kuwa raia wake wameuawa.
Ujumbe wa kundi la Ansaru ulionyesha picha za miili ya watu walioonekana kama mateka hao, raia mmoja wa Uingereza, mtaliano, raia wa Ugiriki na wafanyakazi wanne wa Lebanon. Kundi hilo lilisema kuwa waliwaua kwa sababu ya jaribio la majeshi ya Uingereza na Nigeria kuwaokoa Lakini katika taarifa yake, wizara ya mambo ya nje ya Italia, ilisema kuwa hapakuwa na jaribio lolote la kijeshi kuwaokoa mateka hao kutoka kwa serikali yoyote husika.
Taarifa hiyo iliongeza kuwa kundi hilo halina sababu yoyote ya kuwaua mateka isipokuwa kufanya unyama. Uingereza ilisema kuwa ndege zake za kijeshi zilizoonekana nchini Nigeria zilikuwa huko kuwabeba wanajeshi wanaopigana dhidi ya wapiganaji wa kiisilamu nchini Mali wala sio kuwaokoa mateka.  Kundi hilo lilibuniwa Januari mwaka jana na ni moja ya makundi yanayotajwa kama kundi la kigaidi na serikali ya Uingereza na ambalo limehusishwa na wapiganaji wa al-Qaeda. Kundi hilo lilimteka nyara raia mmoja wa Ufaransa, Francis Colump mwezi Disemba katika jimbo la Katsina. Mnamo Januari, Ansaru lilisema kuwa llifanya shambulizi lililowaua raia wawili wa Nigeria, walipokuwa wanajiandaa kwenda Mali kusaidia katika harakati za kijeshi dhidi ya wapiganaji wa kiisilamu.

No comments:

Post a Comment

TUPE MAWAZO YAKO