Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Oman amesema kuwa, Iran ina nafasi muhimu mno katika matukio ya Mashariki ya Kati na kwamba, nafasi ya Tehran katika kutatua changamoto zinazolikabili eneo hili ni chanya na isiyokanushika. Yusuf bin Allawi amesema hayo mjini Mascut Oman katika mazungumzo yake na Ramin Mehmanparast, msemaji wa Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Iran na kusisitiza kwamba, kuweko fikra moja na ushirikiano wa nchi za Mashariki ya Kati ikiwemo Iran na Oman ni mambo ya dharura katika kuzipatia ufumbuzi changamoto zinazolikabili eneo hili. Yusuf bin Alawi amesema, uhusiano wa Iran na Oman ni wa kirafiki na kidugu na kuongeza kwamba, viongozi wa Tehran na Muscut wana azma thabiti ya kupanua zaidi ushirikiano wa nchi zao katika nyuga mbalimbali. Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Oman amebainisha kwamba, nchi yake inaunga mkono suala la mazungumzo kwa ajili ya kuipatia ufumbuzi kadhia ya miradi ya nyuklia ya Iran. Kwa upande wake Ramin Mehmanparast, Msemaji wa Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Iran amelaani njama za maadui za kuzusha fitina na mifarakano baina ya Waislamu pamoja na njama zao za kila leo za kuuonesha Uislamu kuwa ni tishio.
No comments:
Post a Comment
TUPE MAWAZO YAKO