Monday, March 11, 2013

TALIBAN WAZUNGUMZA NA MAREKANI

Rais Hamid Karzai wa Afghanistan amesema Taliban wa nchi hiyo wako katika mazungumzo na Marekani katika taifa la Ghuba la Qatar,lakini kundi hilo la wanamgambo na Marekani wamekanusha kwamba wameanza tena mazungumzo yao.Karzai ameuambia mkutano wa kuadhimisha Siku ya Kimataifa ya Wanawake kwamba viongozi waandamizi wa Taliban na Wamarekani wamekuwa wakifanya mazungumzo hayo kila siku katika taifa hilo la Ghuba. Taarifa za Marekani zinasema Taliban ilisitisha mazungumzo hayo mwaka mmoja uliopita na kulaumu kwamba yalikuwa yakiyumba,hayatabiriki na hayana uhakika.Serikali ya Marekani imesema imeendelea kujizatiti kufikia usuluhishi wa kisiasa wenye kuhusisha mazungumzo na Taliban lakini maendeleo ya mazungumzo hayo yatahitaji makubaliano kati ya serikali ya Afghanistan na waasi hao. Alipotakiwa kuzungumzia matamshi hayo ya Karzai afisa wa Marekani aliekataa kutajwa jina lake amesema jambo hilo sio kweli na kwamba wanaendelea kuunga mkono mchakato wa usuluhishi wa kisiasa unaoongozwa na serikali ya Afghanistan.Taliban pia imekanusha vikali matamshi hayo ya Karzai na kusema kwamba hakuna maendeleo yoyote yaliofikiwa tokea yalipositishwa.

No comments:

Post a Comment

TUPE MAWAZO YAKO