Monday, March 11, 2013

UTULIVU WAANZA KUPOTEA KATI YA PALESTINA NA ISRAEL


Kiongozi mmoja wa harakati ya Jihadul Islami ya Palestina amesema kuwa, hatua ya utawala wa Kizayuni wa Israel ya kuendelea kufanya jinai dhidi ya Wapalestina zikiwemo jinai zake za hivi karibu katika Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan zinaonesha kuwa zama za utulivu kati ya Wapalestina na Wazayuni zimeisha. Bw. Ahmad al Mudallil amesema hayo katika mahojiano maalumu aliyofanyiwa na televisheni ya al Alam na kusema kuwa, utawala wa Kizayuni ndio utakaobeba lawama zote za yatakayotokea baadaye kutokana na jinai zake katika msikiti wa al Aqsa na kwamba majibu hayatatoka kwa Wapalestina pekee basi yatatoka kona mbalimbali za dunia.
Amesema, adui Mzayuni ni adui mtenda jinai asiye na chembe ya ubinaadamu na hiyo ndiyo dhati yake tangu alipouteka msikiti wa al Aqsa na mji mtukufu wa Baytul Muqaddas na kwamba jinai zake dhidi ya kibla cha kwanza cha Waislamu zinaendelea tangu mwaka 1967. Itakumbukwa kuwa Wapalestina 35 wamejeruhiwa ndani ya Msikiti Mtakatifu wa al Aqsa baada ya wanajeshi wa Israel kuvamia kibla hicho cha kwanza cha Waislamu ili kuwakandamiza Waislamu wa Palestina waliokuwa wanalalamikia jinai ya mwanajeshi mmoja wa Israel ya kuivunjia heshima Qur'ani Tukufu wiki iliyopita.

No comments:

Post a Comment

TUPE MAWAZO YAKO