Tuesday, March 12, 2013

WAISREAL NA MAREKANI WAFANYA NJAMA ZA KUWAZUIA WAKIMBIZI WA KIPALESTINA KURUDI KWAO


Gazeti la Kizayuni la Urshalim Post limeripoti habari ya kuweko harakati mpya za utawala ghasibu wa Israel zenye shabaha ya kufuta haki ya kurejea makwao wakimbizi wa Kipalestina. Gazeti hilo limefichua katika nakala yake ya hivi karibuni kabisa kwamba, Israel imeanzisha harakati mpya katika Umoja wa Mataifa ili haki ya kurejea makwao wakimbizi wa Kipalestina ifutwe na kuondolewa. Kwa mujibu wa gazeti hilo, viongozi wa Israel wanafanya njama kupitia Umoja wa Mataifa pamoja na asasi zinazofungamana na umoja huo ili kubadilisha maana ya "Mkimbizi wa Kipalestina" na hivyo kuwapokonya sifa ya ukimbizi Wapalestina ambao walifukuzwa katika nyumba zao na utawala wa Kizayuni wa Israel.
Ukweli wa mambo ni kuwa, harakati hizi sio mpya kwani huko nyuma utawala wa Kizayuni wa Israel umewahi kuwatumia wajumbe wa Congresi ya Marekani ili kubadilisha na kuwapokonya Wapalestina haki ya ukimbizi. Hata hivyo wakati huo mpango huo mchafu ulikwama kutokana na radiamali kali iliyooneshwa na Wapalestina. Hivi sasa Israel ambayo inapata uungaji mkono wa kila namna wa Marekani inafanya tena harakati za kuhakikisha kwamba, Wapalestina wanapokonywa haki zao zote ikiwemo haki ya kurejea makwao wakimbizi wa Kipalestina. Siasa za kuwafanya kuwa wakimbizi wananchi wa Palestina, daima zimekuwa zikitekelezwa na utawala wa Kizayuni wa Israel kwa lengo la kuimarisha nafasi yake katika ardhi za Wapalestina unazozikalia kwa mabavu. Daima Israel imekuwa ikipata uungaji mkono wa madola ya Magharibi na imekuwa ikitekeleza siasa za kuwafukuza Wapalestina kutoka katika ardhi zao kwa shabaha ya kuvuruga muundo wa kijamii kwenye maeneo unayoyakalia kwa mabavu. Natija ya siasa hizo zilizo dhidi ya utu na ubinaadamu ni Wapalestina kuwa wakimbizi kwa mamilioni. Takwimu zinaonesha kuwa, kuna wakimbizi milioni tano na nusu wa Kipalestina katika nchi mbalimbali duniani. Kuweko idadi kubwa ya wakimbizi wa Kipalestina kunaonesha ukubwa wa maafa waliotwishwa Wapalestina hao na utawala wa Kizayuni wa Israel. Madola ya Magharibi hususan Marekani ambayo inahesabiwa kuwa muungaji mkono mkuu wa utawala wa Kizayuni wa Israel imekuwa pamoja na Tel Aviv katika mipango yake ya kutaka kunyimwa haki ya kurejea makwao wakimbizi wa Palestina. Miongoni mwa mipango ya pamoja ya Tel Aviv na Washington ni kuwapatia Wapalestina hao makazi ya kudumu katika nchi wanazoishi kama wakimbizi. Njama mpya za Marekani na utawala wa Kizayuni wa Israel za kuhakikisha wakimbizi wa Kipalestina wanapokonywa haki ya kurejea makwao zinafanyika katika hali ambayo, maazimio ya Umoja wa Mataifa likiwemo azimio nambari 194 la umoja huo limesisitiza kinagaubaga juu ya haki ya wakimbizi wa Kipalestina ya kurejea makwao pamoja na kulipwa fidia.

No comments:

Post a Comment

TUPE MAWAZO YAKO