Mahakama ya Uingereza imetoa hukumu na kusema serikali ya nchi hiyo ilikosea wakati ilipoiwekea vikwazo benki moja ya Iran mwaka 2009 kwa madai ya kuhusika na mpango wa nyuklia wa Iran. Uamuzi huo wa Jumatano ya leo uliakisi uamuzi wa mwezi Januari wa Mahakama Kuu ya Umoja wa Ulaya ambayo ilibatilisha vikwazo dhidi ya Bank Mellat ya Iran. Msemaji wa benki hiyo amesema huenda wakaishtaki serikali ya Uingereza ili kupata fidia ambayo yamkini ikawa zaidi ya paundi nusu bilioni.
Katika uamuzi uliounguwa mkono na aghalabu ya majaji, na kusomwa na Jaji Jonathan Sumption, Mahakama ya Kilele mjini London imesema uamuzi wa kuiwekea vikwazo Bank Mellat ulikuwa wa kiholela, uliokiuka mantiki na uliokiuka misingi ya uadilifu. Wakili Sarosh Zawalla amesema uamuzi huo wa leo ni ushindi kwa Bank Mellat na utawala wa sheria. Marekani na waitifaki wake katika nchi za Magharibi wamekuwa wakiwekea vikwazo mashirika, taasisi na shakhsia wa Iran kwa madai yasiyo na msingi kuhusu miradi ya kuzalisha nishati ya nyuklia ya Iran yenye malengo ya amani.
No comments:
Post a Comment
TUPE MAWAZO YAKO