Thursday, December 27, 2012

NETANYAHU ATUMIA PROPAGANDA DHIDI YA IRAN KATIKA KAMPENI ZAKE


Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu na Avigdor Lieberman Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Utawala huo, aliyetangaza kujiuzulu hivi karibuni kufuatia tuhuma za uhaini, kwa pamoja hapo jana walianzisha rasmi kampeni zao za uchaguzi katika ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu.
Katika sherehe za ufunguzi wa kampeni hizo za muungano wa chama cha Likud na Beitenu, Netanyahu alizungumzia changamoto kubwa mbalimbali zinazoikabili Israel, sambamba na kuashiria kadhia ya nyuklia yenye malengo ya amani ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. Netanyahu pia aligusia maudhui nyingine ukiwemo uwezo wa kijeshi wa Harakati ya Hizbullah ya Lebanon na Hamas ya Palestina, kadhia ya kuanguka madikteta katika eneo Mashariki na Kati ya kaskazini mwa Afrika, taathira ambayo imesababishwa na mabadiliko ya kisiasa katika eneo hilo na mporomoko wa uhusiano wa baadhi ya watawala wa Kiarabu na Israel. Aidha ameutaja mwako wa Kiislamu kuwa chanzo cha kuenea kwa Uislamu wa kupindukia mipaka katika Mashariki ya Kati na kuongeza kuwa, baadhi ya watu wanasema kuwa, katika kukabiliana na wimbi hili lazima kusalimu amri na kuinua juu bendera ya amani lakini kwamba Israel haitafanya hivyo chini ya uongozi wake.
Katika miezi ya hivi karibuni Waziri Mkuu huyo wa Utawala haramu wa Israel amefanya juhudi kubwa za kuimarisha nafasi yake iliyodhoofika. Lengo la hotuba yake hiyo, ni kujaribu kuvutia kura na kuzidisha nafasi ya ushindi wa chama cha mrengo wa kulia katika uchaguzi unaotarajiwa kufanyika tarehe 22 Januari mwakani. Ni katika hali hiyo ndio maana kiongozi huyo akafanya njama za ziada za kueneza uvumi na uongo dhidi ya miradi ya kuzalisha nishati ya  nyuklia nchini Iran.
Mfumo huo wa kampeni za Israel unashabihiana sana na stratijia zilizotumiwa na wagombea urais katika kampeni za uchaguzi wa hivi karibuni nchini Marekani, kuhusiana na maudhui ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. Itakumbukwa kuwa katika kikao cha hivi karibuni cha Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, Waziri Mkuu huyo wa Utawala wa Kizayuni wa Israel pia aliwasilisha mchoro wa bomu kwa ajili ya kuonyesha kuwa shughuli za nyuklia za Iran ni tishio kwa usalama wa dunia. Hata hivyo njama hiyo haikuungwa mkono na wajumbe wa baraza hilo na badala yake waziri mkuu huyo akaonekana kama mcheza  tamthilia katika siasa za kimataifa.
Aidha hivi karibuni pia akiwa mbele ya Wazayuni katika hafla ya kumbukumbu ya kuuawa Waziri Mkuu wa zamani wa Israel Ishaq Rabin, Netanyahu alidai kuwa, kwa miaka kadhaa shughuli za nyuklia za Iran zimekuwa zikifanyika kwa malengo ya kijeshi huku ikiendelea kuyafadhili makundi aliyoyataja kuwa ya kigaidi nchini Lebanon na huko katika Ukanda wa Gaza.
Wakati kiongozi huyo mwenye misimamo mikali wa utawala katili wa Kizayuni akizizungumzia shughuli za nyuklia za Iran zenye malengo ya amani, fikra za walimwengu zinauona utawala huo wa Israel kuwa ndio tishio kubwa kwa usalama wa dunia, kutokana na kumiliki kwa uchache vichwa vya silaha za atomiki mia tatu 300 katika vituo vyake vya nyuklia.

No comments:

Post a Comment

TUPE MAWAZO YAKO