Wednesday, December 26, 2012

WAPALESTINA WAIONYA TENA ISRAEL JUU YA MAKUBALIANO

Utawala wa Kizayuni wa Israel umeendelea kuvunja makubaliano ya kusimamisha vita huko Ghaza. Makundi ya Palestina likiwemo la HAMAS yametoa onyo kali kwa utawala huo dhalimu na kusisitiza kuwa Israel ndiyo itakayokuja kulaumiwa wakati makubaliano ya kusimamisha vita yatakapovunjika. Musa Abu Marzuq, Naibu wa Mkuu wa Ofisi ya Kisiasa ya Hamas ameonya kuwa itafika wakati makundi ya Palestina yatalazimika kujibu uchokozi wa mara kwa mara wa utawala wa Kizayuni wa Israel na huo ndio utakaokuwa mwisho wa makubaliano ya hivi sasa ya kusimamisha vita. Kwa mujibu wa makubaliano yaliyopelekea kusimamishwa vita vya siku nane vilivyoanzishwa na utawala wa Kizayuni huko Ghaza, Israel iliahidi kuheshimu vipengee vya makubaliano hayo kama vile kuacha chokochoko zake dhidi ya Wapalestina na kufungua vivuko vyote vya kuingia na kutoka Ghaza, hata hivyo hakuna kipengee hata kimoja kilichoheshimiwa na utawala wa Kizayuni. Mwezi uliopita wa Novemba, utawala wa Kizayuni ulilazimika kusimamisha mashambulizi yake huko Ghaza siku nane baada ya kuanzisha mashambulizi hayo kutokana na kukabiliwa na mashambulizi ya mamia ya makombora ya wanamapambano wa Palestina. Takwimu zinaonyesha kuwa Wazayuni walishindwa vibaya kiasi kwamba viongozi kadhaa wa utawala wa Kizayuni wamejiuzulu. Ushahidi mwingine unaoonyesha kuwa Israel haikutarajia kupata majibu makali kutoka kwa Wapalestina ni ile hatua yake ya kufanya haraka kukubali masharti ya Wapalestina katika makubaliano ya kusimamisha vita hivyo. Hata hivyo na kama ilivyotarajiwa, Israel haijaheshimu kabisa vipengee vya makubaliano hayo. Hadi hivi sasa haijafungua vivuko vya kuingia na kutoka Ghaza, inaendelea kuuzingira ukanda huo, inafanya chokochoko za mara kwa mara na vitendo vingine mbalimbali vya kuwachochea Wapalestina. Wachambuzi wa mambo wanaamini kuwa kitendo cha utawala wa Kizayuni cha kutoheshimu makubaliano hayo ni kujaribu kujionyesha kuwa bado una nguvu baada ya kupata fedheha ya kukubali masharti ya watu waliozingirwa kila upande kwa miaka kadhaa licha ya Israel kujidai kuwa ni  moja ya madola yenye jeshi kubwa na kali zaidi duniani. Si hayo tu, lakini pia ripoti zinasema kuwa Israel imeshadidisha mateso yake dhidi ya mateka wa Kipalestina na inaendelea kiujeuri kujenga vitongoji vya walowezi wa Kizayuni, yote hayo ikiwa ni kutaka kujionyesha kuwa ina nguvu za kufanya inalotaka. Hata hivyo weledi wa mambo wanaamini kuwa Israel ya hivi sasa ni dhaifu sana ikilinganishwa na ya miaka ya huko nyuma. Sambamba na hayo, wanamapambano wa Palestina nao wameonya kutoa majibu makali zaidi dhidi ya utawala wa Kizayuni iwapo utaendelea kuvunja makubaliano ya kusimamisha vita, jambo ambalo bila ya shaka linawatia hofu kubwa walowezi wa Kizayuni.

No comments:

Post a Comment

TUPE MAWAZO YAKO