Thursday, January 31, 2013

UINGEREZA YATUMA JESHI NCHINI MALI


Serikali ya London imethibitisha kwamba imetuma askari wasiopungua 350 nchini Mali na katika nchi jirani na nchi hiyo ya Magharibi mwa Afrika. Waziri wa Ulinzi wa Uingereza Philip Hommond amesisitiza tena bungeni juu ya uungaji mkono kikamilifu wa serikali ya London kwa mashambulizi ya Ufaransa nchini Mali. Awali viongozi wa Uingereza walisema kuwa watatoa msaada wa kilojistiki tu kwa Ufaransa katika mashambulizi yake kijeshi huko Mali. Kupanuliwa ushiriki wa Uingereza katika mashambulizi ya kijeshi nchini Mali kunafanyika katika hali ambayo, wanaharakati wanaopinga vita wanalaani mashambulizi ya kijeshi ya Ufaransa nchini humo na kusema kuwa ni vita vya kikoloni. Vilevile wameitaka serikali ya London iache kuunga mkono vita hivyo. Waziri wa Ulinzi wa Uingereza anajitahidi kuhalalisha hatua ya nchi hiyo ya kutuma majeshi huko magharibi mwa Afrika kwa kuhusisha usalama wa Mali na amani ya nchi za Ulaya. Hammond pia amesisitiza kwamba, Ufaransa tangu ilipoanza mashambulizi ya kijeshi huko Mali Januari 11 haijaungwa mkono na nchi wanachama wa Umoja wa Ulaya.
Waziri wa Ulinzi wa Uingereza alitoa matamshi hayo bungeni baada ya kuzungumza kwa simu na Rais François Hollande wa Ufaransa, ili kujaribu kuisaidia serikali ya Paris ambayo inaonekana kuwa imetengwa na nchi nyingine katika suala hilo. Kabla ya kuishambulia Mali, Ufaransa pia ilijitahidi kuonyesha kuwa eneo la magharibi mwa Afrika la nchi za Mali, Algeria, Mauritania na Niger limekuwa kituo na hifadhi ya makundi yaliyofurutu ada ya kigaidi kama lile la waasi wa Kituareg. Hatua ya Poland ya kutuma wataalamu wa kijeshi nchini Mali pia imetekelezwa kwa kisingizio hicho.
Kwa mujibu wa azimio lililopasishwa na Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuhusu uingiliaji wa kijeshi nchini Mali, operesheni hiyo ilipaswa kutekelezwa chini ya usimamizi wa jumuiya ya kieneo ya Ecowas na Umoja wa Afrika kwa mwongozo wa jeshi la Mali. Licha ya hayo, Ufaransa ambayo inakabiliwa na matatizo ya kiuchumi iliingilia kijeshi mgogoro wa Mali, bila ya kuwasiliana na viongozi wa AU na nchi jirani na Mali. Mwezi Disemba mwaka jana baadhi ya duru zilieleza kuwa kumefanyika mazungumzo ya siri kati ya Marekani na Ufaransa kuhusu hali ya Mali na kuna uwezekano mkubwa ndio yaliyoratibu mashambulizi ya kijeshi ya Paris nchini Mali.
Wakati huo huo Waziri Mkuu wa Uingereza David Cameron amefanya safari nchini Algeria ili kuratibu ushirikiano zaidi na serikali ya Algiers katika kuwasaidia askari wa Ufaransa nchini Mali. Hata hivyo huenda serikali ya Algiers isikubali suala hilo hasa baada ya tukio la utekeaji nyara katika kiwanda cha gesi cha In Amenas uliochochewa na mashambulizi hayo ya Ufaransa nchini Mali.

No comments:

Post a Comment

TUPE MAWAZO YAKO