Thursday, February 21, 2013

IRAN YATENGENEZA RADA YENYE UWEZO WA KILOMITA 3000


Waziri wa Ulinzi wa Iran Brigedia Jenerali Ahmad Vahidi amesema kuwa Jamhuri ya Kiislamu sasa inatengeneza mifumo ya rada za masafa marefu zenye uwezo kulinda usalama wa masafa ya kilomita 3000.
Vahidi amesema hayo leo Jumanne na kuongeza kwamba, Iran imekuwa ikitengeneza kwa wingi rada za kijeshi zenye uwezo wa wigo wa kilomita 500-700 na sasa inatengeneza rada mpya zenye wigo wa kilomita 1000 hadi 3000.
Waziri wa Ulinzi wa Iran amesema, baadhi ya rada hizo zilizotengenezwa hapa nchini zitatumika pia kutafuta satalaiti zilizoko kwenye anga za mbali.
Vahidi ameongeza kuwa hivi karibuni Iran itazindua rada za kisasa, manowari mpya za kivita, boti zenye uwezo wa kupaa na nyambizi za kisasa kabisa. Mapema jana Jumatatu Vahidi alitangaza kuwa hivi karibuni Iran itaonyesha ndege mpya zisizo na rubani au drone zenye uwezo mkubwa wa kivita na kiupelelezi.
Katika miaka ya hivi karibuni Iran imepata mafanikio makubwa katika sekta ya kujihami na imeweza kujitosheleza katika uzalishaji wa zana muhimu za kivita. Iran imesisitiza kuwa uwezo wake mkubwa wa kijeshi umejengeka katika msingi wa kujihami na si tishio kwa nchi nyingine.

No comments:

Post a Comment

TUPE MAWAZO YAKO