Saturday, February 23, 2013

MAREKANI YAIONYA IRAN JUU YA NYUKLIA

Marekani imeionya Iran kuacha vitendo vya uchukozi kufuatia ripoti kuwa inauendeleza mpango wake wa nyuklia. Shirika la Nguvu za Atomiki Duniani, IAEA, limesema kuwa Iran imeanza kuweka vifaa vya kuchuja mionzi ya nyuklia katika moja ya vinu vyake. Vifaa hivyo vinaaminika kuwa bado havijaanza kufanyakazi. Mara vitakapoanza kufanya kazi, vifaa hivyo vitaiwezesha Iran kufanya kazi zake za nyuklia kwa kasi kiasi cha kupata malighafi ambazo mataifa ya magharibi yanahofia zinaweza kutumikia kutengeneza silaha za nyuklia. Hata hivyo Iran imeendelea kusisitiza kuwa mpango wake huo wa nyuklia ni kwa ajili ya matumizi ya kawaida. Ripoti ya IAEA imetolewa ikiwa ni siku chache kabla ya kuanza mazungumzo baina ya Iran na mataifa yenye nguvu duniani ikiwemo Ujerumani. Mkutano huo utakuwa wa kwanza tangu kufanyika mazungumzo ya awamu tatu yaliyofanyika Juni mwaka jana.

No comments:

Post a Comment

TUPE MAWAZO YAKO