Sunday, February 03, 2013

MPANGO WA BIDDEN KUTATUA MZOZO WA NYUKLIA WA IRAN


Rais Barack Obama wa Marekani amesisitiza katika duru yake ya pili ya urais nchini humo juu ya udiplomasia wa "mashinikizo na vikwazo" na amempa makamu wake Jo Biden jukumu la kufuatilia kadhia ya nyuklia ya Iran. Biden ambaye ameelekea Munich, Ujerumani kwa ajili ya kushiriki katika kikao cha usalama, ameeleza kuwa nchi yake iko tayari kufanya mazungumzo ya moja kwa moja na Iran na kwamba Washington ina mpango ambao kwa mujibu wa madai yake unaweza ukafungua njia ya kutatuliwa kidiplomasia kadhia ya nyuklia ya Iran. Biden amesema pia kuwa Marekani haitairuhusu Iran kumiliki silaha za nyuklia na kwamba mlango wa mazungumzo ya amani na Tehran hautakuwa wazi milele. 
Matamshi hayo ya Joe Biden yamekaribishwa na kuungwa mkono na viongozi wa Umoja wa Ulaya akiwemo Catherine Ashton, Mkuu wa Siasa za Nje wa umoja huo na Guido Westewelle, Waziri wa Mambo ya Nje wa Ujerumani. Matamshi ya kiongozi huyo wa White House yanaonesha kwamba Marekani inaendeleza siasa zake za propaganda chafu dhidi ya Iran na kwamba Tehran kwa mujibu wa mtazamo wa Wamagharibi, ni mtuhumiwa mkubwa; kwa sababu hiyo mazungumzo ya aina yoyote ile na Iran yanapaswa kufanyika kwa mujibu wa madai hayo yasiyo na msingi. Kwa hakika hatua hiyo ya Marekani ina lengo la kuidhihirisha serikali ya Washington kuwa ina nia njema ya kutaka kutatua kadhia ya nyuklia ya Iran kwa njia za kidiplomasia.
Ukweli wa mambo ni kuwa Marekani na utawala wa Kizayuni wa Israel zimepanga njama kabambe na harakati kubwa kwa ajili ya kikao cha Munich na zinafanya juhudi ili kunufaika na fursa hiyo dhidi ya miradi ya kuzalisha nishati ya nyuklia ya Iran. Ni kwa sababu hiyo ndio maana katika hotuba yake kwenye mkutano wa Munich, Makamu wa Rais wa Marekani amefanya jitihada kubwa za kuchafua sura ya Iran badala ya kuzungumzia haki za nyuklia za Jamhuri ya Kiislamu.   Hii ni katika hali ambayo viongozi wa Iran wamekosoa vikali suala la kubadilishwa mahali na tarehe ya kufanyika mazungumzo kati ya Tehran na kundi la 5+1 na hatua ya nchi za Magharibi ya kuchapisha habari za uwongo kuhusiana na suala hilo. Tangu karibu miezi 8 iliyopita yaani tangu baada ya kikao cha Moscow, Iran ilikuwa imejiandaa kufanya duru mpya ya mazungumzo, lakini upande wa Magharibi umekataa kuketi kwenye meza ya mazungumzo kwa sababu ambazo Iran pia haizijui.
Suala kuu hapa si wakati wa kufanyika mazungumzo hayo wala mahala gani yatafanyika, bali ni jambo jingine ambalo ni kuwa, baadhi ya wanachama wa kundi la 5+1 hawako tayari kufanya mazungumzo hayo. Viongozi wa Marekani wameelewa kuwa Russia na China hazichezi tena katika uwanja wa udiplomasia wa Magharibi kama ilivyokuwa huko nyuma na migongano ya mitazamo ya Kremlin na Peking na ile ya Marekani imepanuka na kugusa masuala mengi kuanzia mgogoro wa Syria hadi kadhia ya nyuklia ya Iran. Kwa sababu hiyo maafisa wa serikali ya Marekani wametoa fikra ya kufanyika mazungumzo ya moja kwa moja na Iran. Hatua hiyo imechukuliwa kwa sababu kadhaa. Kwanza ni kuwa Marekani na baadhi ya waitifaki wake wa Ulaya walitarajia kuwa vikwazo vyao dhidi ya Iran vitazusha uasi na machafuko ya kijamii. Hata hivyo badala ya kuwafanya wananchi wa Iran waichukie serikali na mfumo wao, vikwazo hivyo vimewafanya wazichukie zaidi nchi za Magharibi.
Sababu ya pili ni kuwa tofauti na makelele yake ya kipropaganda, Marekani haijaweza kubuni stratijia ya maana kwa ajili ya kuanza mazungumzo na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. Hii ni kwa sababu tunapotazama mwenendo wa Marekani kuhusu Iran tutatambua kuwa madai ya kutaka kufanya mazungumzo ya moja kwa moja na Tehran hayana maana yoyote. Ukweli ni kuwa lengo la Marekani katika harakati yake hiyo ni kutaka kubadili mlingano wa kimataifa kuhusu suala la mazungumzo na Iran. Duru za kisiasa za nchi za Magharibi pia zinatumia propaganda za vyombo vya habari kuonesha kuwa Iran haiko tayari kufanya mazungumzo na kwa njia hiyo itambulike kuwa ni tishio kwa jamii ya kimataifa.      

No comments:

Post a Comment

TUPE MAWAZO YAKO