Thursday, March 28, 2013

HAMAS YATOA TAHADHARI KWA ISRAEL JUU YA MASJIDUL AQSAA


Katika radiamali yake kuhusiana na wito uliotolewa na mwakilishi  mmoja wa Bunge la Israel (Knesset)  kwa Wazayuni wa kusherehekea sikukuu ya Kiyahudi katika msikiti wa al Aqsa, Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina (Hamas) imewatahadharisha viongozi wa utawala huo na kuwataka wajiepushe na hatua hiyo ya kishenzi.
Sambamba na kulaani wito huo wa Moshe Feiglin mwakilishi wa Bunge la Israel kwa Wazayuni wa kusherehekea sikukuu ya Kiyahudi ya 'Pasaka'  katika msikiti wa al Aqsa, Hamas imezitaka nchi za Kiislamu na taifa la Palestina kukabiliana na mpango  huo wa kidhulma wa adui Mzayuni wa kutaka kuhujumu msikiti huo. Hamas pia imetahadharisha kwamba Wazayuni ndio watakaobeba lawama na taathira mbaya za kusherehekea Pasaka katika Msikiti wa al Aqsa ambao ni kibla cha mwanzo cha Waislamu. Awali Taasisi ya Wakfu na Turathi ya al Aqsa pia ilitahadharisha juu ya athari mbaya za kusherehekea Pasaka katika msikiti huo na kutaka jamii ya kimataifa hasa nchi za Kiislamu na Kiarabu zichukuwe hatua za haraka na zenye taathira za kukabiliana na jinai na hujuma za Wazayuni dhidi ya msikiti huo zinazozidi kila uchao.
Hivi karibuni askari na walowezi wa Kizayuni wamekuwa wakijikusanya kwenye ua wa Masjidul Aqsa kwa lengo la kuingia kwenye msikiti huo mtukufu, ambapo Wapalestina walizima njama hizo. Walowezi wa Kizayuni na Wazayuni wenye misimamo mikali kwa visingizio tofauti kama kusherehekea sikukuu ya kidini ya Pasaka, siku zote wamekuwa wakitaka kuhujumu Msikiti wa al Aqsa na Baitul Muqaddas. Wazayuni wenye misimamo ya kufurutu ada wanaosaidiwa na askari wa Israel wanaendelea kuhujumu maeneo matakatifu ukiwemo Msikiti wa al Aqsa huku nchi za Kiarabu zikinyamazia jinai hiyo na kuishia tu kutoa maneno matupu. Kuhusu suala hilo viongozi wa Jumuiya ya Nchi za Kiarabu katika mkutano wao wa 24 uliofanyika Jumanne nchini Qatar, walichukuwa hatua ya kimaonyesho tu wakiitaka Israel iondoe vitongoji vya walowezi wa Kizayuni katika ardhi za Palestina na kuacha kuhujumu Msikiti wa al Aqsa.
Nchi za Kiarabu zinanyamazia kimya hujuma za Wazayuni dhidi ya msikiti huo na kadhia nzima ya Palestina, katika hali ambayo hujuma zinazokaririwa na askari wa Kizayuni dhidi ya msikiti huo wa kihistoria, msikiti wa Qubbatus Swakhra na makanisa katika mji wa Quds Sharif zimekuwa zikilaaniwa na Shirika la Elimu, Sayansi na Utamaduni la Umoja wa Mataifa (UNESCO). Zaidi ya hayo vitongoji vya walowezi wa Kizayuni vilivyojengwa katika ardhi za Palestina vimekuwa vikipingwa na kukosolewa na jamii ya kimataifa. Kwa kuzingatia hayo inaonekana kuwa, njia pekee iliyobakia ni taasisi za kimataifa kutafuta suluhisho la kudumu litakalozuia kuendelea siasa za utawala wa Kizayuni za kupenda kujitanua katika ardhi za Palestina.

No comments:

Post a Comment

TUPE MAWAZO YAKO