Harakati ya Mapambano ya Hizbullah ya Lebanon imelaani matamshi ya Rais Barack Obama wa Marekani kwamba harakati hiyo iaridhiwe kwenye orodha ya makundi ya kigaidi. Hizbullah imesema kwenye taarifa yake kwamba, Obama ni kibaraka wa Wazayuni maghasibu na wala si mwanadiplomasia kama vinavyonadi vyombo vya habari vya Magharibi.
Taarifa hiyo aidha imesema kuwa, matamshi ya Obama yamefuta kabisa uwezekano wa kutumiwa mazungumzo kama njia ya kutatua mgogoro wa Mashariki ya Kati na kwamba Muqawama ndio njia ya pekee ya kupata ushindi.
Huku hayo yakijiri, Rais Obama amemaliza ziara yake ya siku tatu katika utawala wa Kizayuni wa Israel na huko Palestina inayokaliwa kwa mabavu na Israel. Rais huyo wa Marekani ameelekea Jordan anakotarajiwa kukutana na Mfalme Abdallah II. Kadhia ya Syria inatarajiwa kutawala mazungumzo kati ya viongozi hao. Weledi wa mambo wanaamini kuwa safari ya Obama huko Israel na Palestina ilikuwa ya kimaonyesho tu na lengo kuu lilikuwa ni kuhuisha uhusiano wake na Benjamin Netanyahu ambao ulikumbwa na misukosuko katika kipindi chake cha kwanza cha uongozi. Baadhi ya wachambuzi wamesema hatua ya Obama ya kwenda Palestina inayokaliwa kwa mabavu mikono mitupu ni kejeli kwa Wananchi wanaoendelea kuishi kwa hofu kutokana na jinai za kila leo za Israel.
No comments:
Post a Comment
TUPE MAWAZO YAKO