Wednesday, March 27, 2013

KOREA YASEMA VITA YA NYUKLIA INAKARIBIA

Wizara ya Mambo ya Nje ya Korea Kaskazini imetoa taarifa kwa Umoja wa Mataifa ikisema vita vya nyuklia vinanukia katika Peninsula ya Korea. Taarifa ya Pyongyang kwa Umoja huo inasema kuwa, Marekani na Korea Kusini zinaendelea na chokochoko katika eneo hilo; jambo linalotishia kuanza kwa vita vya silaha za nyuklia. Taarifa hiyo pia imesisitiza kuwa, Korea Kaskazini itatumia kila njia kulinda ardhi na uhuru wake hata kama italazimika kutumia makombora ya nyuklia. Vitisho hivyo vimetajwa kuwa hatari zaidi kuwahi kutolewa na Pyongyang na kutokana na hali hiyo, Marekani imetangaza kuwa imeimarisha ngao zake dhidi ya makombora ili kukabiliana na vitisho hivyo. Majuma mawili yaliyopita, Korea Kaskazini ilitishia kuzishambulia Marekani na Korea Kusini kutokana na nchi mbili hizo kufanya maneva ya pamoja ya kijeshi katika Peninsula ya Korea. Pyongyang ilisema maneva hayo ni tangazo la moja kwa moja la vita dhidi yake. Tayari Korea Kaskazini imejiondoa kwenye mkataba wa usitishaji vita wa mwaka 1953 uliohitimisha vita kati yake na nchi jirani ya Korea Kusini.

No comments:

Post a Comment

TUPE MAWAZO YAKO