Tuesday, March 05, 2013

NETANYAHU ATANGAZA KUSHINDWA KUUNDA BARAZA LA MAWAZIRI

Siku ya Jumamosi ya tarehe Pili Machi, Benjamin Netanyahu, Waziri Mkuu wa utawala wa Kizayuni, alitangaza rasmi kushindwa kwake kuunda Baraza la Mawaziri la serikali ya mseto. Pamoja na kupewa fursa ya siku 28 kuhakikisha anakamilisha kazi hiyo, Netanyahu ameshindwa kuvikinaisha vyama vya kisiasa kujiunga na serikali yake ya mseto. Baada ya kushindwa huko kwa Waziri Mkuu huyo mwenye misimamo ya kuchupa mipaka, alikwenda kwenye makazi ya Shimon Peres, Rais wa utawala pandikizi wa Israel na kumuomba amuongezee muhula mwengine wa wiki mbili, ombi lililokubaliwa na rais huyo. Hivi sasa Netanyahu ana fursa ya wiki mbili tu kuhakikisha anaunda serikali hiyo ya mseto. Ikiwa Benjamin Netanyahu hakuweza kuunda serikali hiyo katika kipindi hicho, kwa kawaida Rais wa utawala wa Kizayuni kwa kushauriana na Bunge, humchagua kiongozi wa chama ambacho kilishika nafasi ya pili katika uchaguzi na kumpa jukumu la kuunda serikali hiyo. Kiongozi huyo naye hupewa muhula wa wiki nne sawa na siku 28 kuhakikisha anaunda serikali hiyo ya mseto. Iwapo atashindwa kufanya hivyo katika kipindi alicyopewa, basi rais wa utawala huo haramu wa Israel anaweza kutoa amri ya kuitishwa uchaguzi mwingine. Katika uchaguzi wa bunge uliofanyika mwezi Januari huko katika ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu, muungano wa vyama vya Likud-Yisrael Beiteinu vya Benjamin Nentanyahu na Avigdor Lieberman vilipata viti 31 kati ya viti vyote 120 vya bunge la utawala huo na hivyo kuwa na haki ya kuteua Waziri Mkuu. Kwa mujibu wa sheria za uchaguzi za utawala haramu wa Israel, kiongozi wa chama kilichoibuka na ushindi katika uchaguzi, huwa na fursa ya wiki sita na nyongeza ya wiki mbili ya kuhakikisha anaunda serikali. Hadi sasa zimepita wiki nne huku Benjamin Netanyahu Mkuu wa Chama cha Likud akiwa ameweza kuungana na chama kimoja tu cha Movement, kinachoongozwa na Tzipi Livni. Chama cha Movement kina viti sita tu katika bunge la utawala wa Kizayuni. Aidha Netanyahu hivi sasa anatakiwa kuvishawishi vyama viwili vingine kikiwemo cha Jewish Homekinachoongozwa na Naftali Bennett na chama cha Future kinachoongozwa na Yair Lapid vishirikiane na Likud kuunda serikali. Vyama hivyo viwili kwa pamoja vina viti 31 katika bunge la utawala huo. Hata hivyo vyama hivyo vimekataa kujiunga na Netanyahu. Tofauti zilizopo kati yao na Tzipi Livni, zimepelekea vyama hivyo kukataa kujiunga na serikali hiyo. Tofauti hizo zimeongezeka kiasi cha kuenea habari zilizonyuma ya pazia za kwamba, viongozi wa vyama hivyo wamekubaliana kumng'oa madarakani Benjamin Netanyahu. Hali imekuwa ngumu sana kiasi kwamba Waziri Mkuu huyo wa utawala wa Kiayuni amelazimika kujiunga na wapinzani wake wakuu. Hivi karibuni Netanyahu alimtaka Shelly Yachimovich, kiongozi wa chama cha Israeli Labor, kujiunga na Baraza lake la Mawaziri. Ni vyema kuashiria hapa kwamba, Yachimovich na chama chake cha mrengo wa kushoto, ni moja ya wapinzani wakubwa wa Netanyahu. Ni kwa sababu hiyo ndio maana kimekataa kujiunga na serikali ya Netanyahu. Ukweli ni kuwa, Benjamin Netanyahu anakabiliwa na kazi ngumu ya kuunda serikali ya mseto katika kipindi hiki cha wiki mbili zilizosalia.

No comments:

Post a Comment

TUPE MAWAZO YAKO