Wednesday, March 27, 2013

RUSSIA YAITAKA LEBANON KUTATUA MATATIZO YAKE WENYEWE

Serikali ya Russia imewataka Walebanon kuzuia uingiliaji wa aina yoyote ile wa madola ya kigeni katika mambo ya ndani ya nchi hiyo. Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Russia Alexander Lukashevich ameyasema hayo leo na kusisitiza kuwa, nchi yake inaamini kwamba, Walebanon lazima watatue matatizo ya taifa lao wao wenyewe kwa njia za mazungumzo, likiwamo suala la uundwaji wa serikali mpya na kufanyika uchaguzi wa bunge na wasitoe mwanya kwa wageni kuingilia mambo ya ndani ya nchi hiyo. Aidha ripoti hiyo imesisitiza kuwa, suala la usalama na utulivu nchini Lebanon ni jambo ambalo linapaswa kupewa kipaumbele na kwamba, taifa hilo la Kiarabu lazima lichukue hatua za lazima zitakazoiletea maslahi nchi hiyo na kusaidia demokrasia ya kweli na kuhakikisha usalama na ustawi unapatikana nchini humo. Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Russia piaamesema kuwa, nchi yake inaunga mkono haki ya kujitawala, uhuru wa nchi na juhudi zote zinazofanywa na makundi ya kisiasa na kidini ya Lebanon katika kukabiliana na changamoto zinazoikabili nchi hiyo hivi sasa. Ni vyema kuashiria hapa kuwa, siku ya Jumamosi, Waziri Mkuu wa Lebanon, Mohammad Najib Mikati, alitangaza kujiuzulu na Rais Michel Suleiman wa nchi hiyo akakubali kujiuzulu kwake.

No comments:

Post a Comment

TUPE MAWAZO YAKO