Wednesday, March 27, 2013

WAFUNGWA WA GUANTANAMO WAUNGWA MKONO

Wanaharakati wa haki za binaadamu katika pembe mbalimbali za dunia wameendelea kuunga mkono mgomo wa chakula wa wafungwa wa jela ya Guantanamo. Kwa mujibu wa ripoti iliyotangazwa na televisheni ya PRESS TV, mgomo wa wanaharakati hao wa haki za binaadamu katika pembe mbalimbali za dunia unafanyika kama ishara ya kuungana na wafungwa hao wanaoendelea kuzuiliwa katika jela ya kutisha ya Guantanamo. Mgomo huo ulianza tarehe 24 Machi na unatarajia kuendelea hadi tarehe 30 ya mwezi huu. Mbali na mgomo huo, wanaharakati hao wamepanga kufanya mikusanyiko kadhaa katika nchi kadhaa katika kuwaunga mkono wafungwa hao. Tarehe 14 mwezi huu mawakili 45 wanaowatetea baadhi ya wafungwa wanaoshikiliwa katika jela hiyo ya Guantanamo walimtumia barua ya wazi Waziri wa Ulinzi wa Marekani Chuck Hagel wakimtaarifu kuhusu suala hilo na kumtaka achukue hatua za haraka ili kumaliza mgomo huo. Wafungwa hao walianza mgomo huo tangu Februari 6 mwaka huu baada ya wafanyakazi wa jela hiyo ya Guantanamo kupora vitu vya wafungwa hao zikiwemo barua, picha na kuzivunjia heshima nakala za kitabu kitukufu cha Qu'rani wakati walipozikagua seli zao.

No comments:

Post a Comment

TUPE MAWAZO YAKO