Saturday, March 02, 2013

RUSSIA YAKOSOA MAAFIKIANO YA ROME


Serikali ya Russia imelaani vikali maamuzi yaliyochukuliwa na nchi za Magharibi ya kuyaunga mkono makundi ya kigaidi nchini Syria. Russia imetangaza kuwa, maamuzi yaliyochukuliwa kwenye kikao kinachodaiwa kuwa cha  'marafiki wa Syria' mjini Rome, yanatoa ushawishi mkubwa kwa  makundi  hayo ya kigaidi kuongeza juhudi zao za kuuangusha utawala wa nchi hiyo. Alexander Lukashevich Msemaji wa Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Russia amesema kuwa, matamshi yaliyotolewa katika kikao cha Roma, yanawashawishi magaidi wenye kufurutu mipaka kuendelea na vitendo vyao vya kigaidi kwa lengo la kutwaa kwa mabavu utawala wa nchi hiyo ya Kiarabu na kufumbia macho machungu na mustakbali wa wananchi wa nchi hiyo.
Nchi kadhaa pamoja na taasisi za kimataifa na kieneo zilishiriki kwenye kikao cha siku moja kilichofanyika Fabruari 28 mjini Rome, kwa lengo la kuwasaidia magaidi nchini Syria. John Kerry Waziri wa Mambo ya Nchi za Nje wa Marekani na viongozi wengine wa ngazi za juu wa nchi 11 duniani wamedai kwenye kikao hicho kwamba wanataka mabadiliko ya mlingano wa kimadaraka nchini humo. Kerry amesema kuwa, Washington imetenga kiasi cha dola milioni 60 kwa lengo la kuwasaidia magaidi nchini Syria na kwamba imeanza kutoa misaada ya moja kwa moja ya kitiba na chakula kwa wapiganaji wa 'jeshi la ukombozi wa Syria' linalopambana na serikali ya Damascus. Mwishoni mwa kikao hicho, Umoja wa Ulaya pia ulilifanyia marekebisho suala la vikwazo vya silaha dhidi ya Syria na kuahidi kuwapatia magaidi zana za kivita na misaada ya kijeshi. Inafaa kuashiria hapa kuwa, mara baada ya kuanza machafuko ya ndani nchini Syria na kubadilika kuwa vita vya wenyewe kwa wenyewe, nchi za Magharibi na hasa Marekani na Uingereza na baadhi ya washirika wao wa Kiarabu, zimekuwa zikifanya njama kubwa za kutaka kuuangusha utawala wa Syria. Njama hizo ni pamoja na kutoa misaada ya kifedha, kilojisiki, kijasusi, kisilaha na hata mafunzo ya kijeshi kwa makundi ya kigaidi nchini humo. Hivi sasa Marekani, Uingereza na Ufaransa zimeshadidisha uungaji mkono wao wa kijasusi na kisilaha kwa lengo la kuongeza wimbi la machafuko na hatimaye kuiangusha serikali ya Rais Bashar Assad wa nchi hiyo. Bila shaka vitendo vinavyotekelezwa hivi sasa na nchi za Magharibi na hasa Marekani na Uingereza kuhusiana na mgogoro wa Syria vinakinzana waziwazi na misimamo ya nchi hizo yapata miaka miwili iliyopita, wakati kilipofanyika kikao cha Umoja wa Mataifa huko Geneva na kutolewa mapendekezo ya kufuatwa njia za amani zenye shabaha ya kuutatua mgogoro wa Syria. Nchi za Magharibi na hasa Marekani na Uingereza na nchi nyingine mithili ya Russia na China ziliunga mkono kikamilifu mpango huo. Nyendo za Marekani na Uingereza kuhusiana na mgogoro wa Syria ambazo zinakosolewa vikali na Russia, zinadhihirisha wazi misimamo ya kindumakuwili ya nchi hizo katika kukabiliana na masuala ya kimataifa. Hii ni katika hali ambayo, Russia na China zikiwa ni nchi wanachama wa kudumu wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa mara kadhaa zimesisitiza misimamo yao ya kutaka kadhia ya Damascus itatuliwe kwa njia za amani. Viongozi wa Russia mara kadhaa wamesisitiza kuwa makubaliano yoyote yatakayofikiwa kitaifa kwa lengo la kutatuliwa mgogoro wa Syria, yanapaswa yazingatie suala la kupokonywa silaha makundi ya kigaidi, kukomeshwa operesheni za kijeshi, kukatwa misaada ya silaha kutoka nchi za kigeni na kuendelezwa mchakato wa serikali ya Damascus wa kuleta mabadiliko ya kisiasa nchini. Hata hivyo, mambo hayo  yanakabiliwa na upinzani mkubwa wa maadui wa Syria na hasa Marekani na waitifaki wake  wa Ulaya na  baadhi ya nchi za Kiarabu. Alaa kulli haal, licha ya mashinikizo ya nchi za Magharibi, Russia bado ina azma ya kuendeleza uungaji mkono wake wa pande zote kwa serikali ya Syria.  

No comments:

Post a Comment

TUPE MAWAZO YAKO