Tuesday, April 09, 2013

NATO YAUA 18 AFGHANISTAN

Watu 18 wameuawa nchini Afghanistan wakiwemo watoto wadogo 11 kufuatia mashambulio ya anga ya vikosi vya Jumuiya ya kijeshi ya NATO mashariki mwa Afghanistan. Wasifullah Wasifi, Msemaji wa Jimbo la Kunar amesema kuwa, mashambulio hayo ya anga ya NATO yamefanywa katika kijiji cha Shighal katika viunga vya jimbo hilo na kwamba, yamefanyika baada ya vikosi hivyo vya NATO na vile vya serikali ya Afghanistan kukabiliwa na mashambulio ya Taliban. Taarifa zaidi kutoka nchini Afghanistan zinasema kuwa, mbali na watoto wadogo, miongoni mwa waliouawa katika mashambulio hayo ya anga ya Jumuiya ya Kijeshi ya NATO wamo wanawake sita. Rais Hamid Karzai wa Afghanistan amelaani vikali mashambulio hayo na ametoa amri ya kufanyika uchunguzi mara moja kuhusiana na mashambulio hayo. Taarifa ya Ikulu ya Rais wa Afghanistan imesisitiza kwamba, serikali yake inalaani operesheni yoyote ile ya kijeshi inayopelekea kuuawa raia wasio na hati yoyote. Mauaji hayo yanakuja siku moja tu baada ya Wamarekani watano kuuawa akiwemo mwanadiplomasia mmoja kijana kufuatia mashambulio mawili tofauti ya Taliban mashariki na kusini mwa nchi hiyo.

No comments:

Post a Comment

TUPE MAWAZO YAKO