Habari za maandamano ya kulalamikia hali ngumu ya maisha katika ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu na utawala haramu wa Israel, zinaendelea kuripotiwa na duru mbalimbali za habari. Kwa mujibu wa gazeti la Kizayuni la Yediot Ahronot, hapo juzi waandamanaji walipiga kambi mbele ya nyumba ya Waziri mpya wa Fedha wa Israel Yair Lapid wakipiga nara kama tunavyonukuu, "Yair, familia za Waisrael zinakabiliwa na njaa" na "acha kuishi katika ulimwengu wa ndoto." Mwisho wa kunukuu. Kuongezeka kwa idadi ya watu wasio na ajira na kupanda kwa gharama za huduma za kijamii ni moja ya sababu zinazopelekea raia wa utawala bandia wa Kizayuni kuandamana kila siku. Mmoja wa waandamanaji hao alihojiwa na gazeti hilo la Yediot Ahronot na kufafanua kuwa, waziri huyo wa fedha wa Israel hapasi kulisahau tabaka la watu wa chini kimaisha. Alisema pia kuwa, raia wa Israel hawapasi kuishi maisha magumu huku waziri huyo wa fedha akiwahudumia tu matajiri na mabwenyenye. Maandamano mbele ya nyumba ya Yair Lapid, yanajiri katika hali ambayo hivi karibuni waziri huyo alikiri juu ya kuzorota kwa hali ya uchumi wa utawala haramu wa Kizayuni na kusisistiza kwamba, hakuna njia nyingine mbala ya kumaliza hali hiyo isipokuwa kufuata hatua ngumu za kubana matumizi ili kuuepusha utawala huo na raia wake kutokana na mgogoro wa kiuchumi. Waziri huyo mpya wa Fedha wa Israel amewataka raia wa Kizayuni kujiandaa kwa ajili ya kukabiliana na hali ngumu zaidi ya kimaisha katika siku za usoni. Hii ni katika hali ambayo tafiti za mwaka 2012 zinaonyesha kwamba, mishahara ya raia wa Israel imepungua kwa asilimia 24 ikilinganishwa na mwaka 2011. Aidha benki kubwa za utawala huo pia zimetoa ripoti inayoonyesha kupata hasara kubwa na kupungua faida ya kibenki katika mwaka uliopita wa 2012. Kufuatia hali hiyo, weledi wa masuala ya kisiasa wanaamini kuwa, hatua ya utawala wa Kizayuni ya kujadili mipango ya kubana matumizi, inaonyesha wazi kiwango cha mgogoro wa kiuchumi unaoukabili utawala huo sambamba na kushindwa viongozi wa Israel kukabiliana na hali hiyo mbaya ya kiuchumi. Alaa kulli hal, kushadidi migogoro na kuharibika kwa hali ya mambo ndani na nje ya utawala wa Kizayuni, kumezifanya duru za utawala huo kuamini kwamba, watawala wa Tel Aviv wanapaswa kuweka wazi mambo sambamba na kukiri ya kwamba, Israel hivi sasa inakabiliwa na mgogoro mkubwa. Aidha mwenendo wa kuongezeka kwa migogoro ya kiuchumi, kisiasa na kijamii ya utawala wa Kizayuni, unaweka wazi ukweli huu kwamba, viongozi wa Israel, wameshindwa kukabiliana na hali hiyo, suala ambalo limepelekea kuongezeka migogoro ya ndani ya utawala huo vamizi. Ukweli ni kwamba, kuongezeka kwa wimbi la kulalamikia hali mbaya ya kiuchumi huko Israel, kunaweka wazi ukweli huu kwamba, utawala huo umeshindwa kutatua matatizo mengi yanayoukabili.
No comments:
Post a Comment
TUPE MAWAZO YAKO