Wednesday, April 10, 2013

UN YASEMA MACHAFUKO YA SYRIA NI KUTOKANA NA SILAHA ZA LIBYA

Ripoti ya Umoja wa Mataifa iliyotolewa jana Jumanne inaeleza kuwa silaha zimekuwa zikienezwa kutoka Libya katika kiwango cha kutisha na kuchochea mizozo huko Mali, Syria na katika maeneo mengine. Taarifa hiyo imesema silaha hizo kutoka Libya zinaimarisha uwezo wa kisilaha wa makundi yenye kufurutu ada na watenda jinai katika eneo. Ripoti ya wataalamu wa Umoja wa Mataifa imeeleza kuwa vikosi vya usalama vya serikali ya Libya ni dhaifu huku makundi yenye silaha yanayoundwa na wapiganaji wa zamani wa nchi hiyo yakiendelea kuwa na nguvu. Ripoti hiyo yenye kurasa 94 ya tarehe 15 Februari lakini iliyochapishwa jana imeeleza kuwa uenezaji wa silaha kutoka Libya unachochea moto wa machafuko yanayoendelea kuziathiri baadhi ya nchi za Kiafrika sambamba na kuimarisha uwezo wa umiliki wa silaha kwa makundi yanayobeba silaha yakiwemo makundi ya kigaidi. Wataalamu wa Umoja wa Mataifa wamesema uhamishaji wa silaha hadi Syria ambako machafuko ya miaka miwili yameua watu zaidi ya elfu sabini uliratibiwa kutoka katika maeneo mbalimbali ya Libya ikiwemo miji ya Misrata na Benghazi kupitia Uturuki au kaskazini mwa Lebanon.

No comments:

Post a Comment

TUPE MAWAZO YAKO