Monday, May 27, 2013

HOTUBA YA KIONGOZI WA HIZBULLAH JUU YA USHINDI WAO DHIDI YA ISRAEL

Tarehe 25 Mei inasadifiana na kumbukumbu ya ushindi wa muqawama dhidi ya Wazayuni na kukombolewa maeneo ya kusini mwa Lebanon. Katibu Mkuu wa Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya nchini Lebanon Hizbullah Sayyid Hassan Nasrullah amehutubia kumbukumbu hizo na kugusia mambo mengi. Sayyid Hassan Nasrullah ameitaja siku ya kukimbia kwa madhila askari vamizi wa Kizayuni katika maeneo ya kusini mwa Lebanon kuwa ni 'Siku ya Mwenyezi Mungu' na kuongeza kuwa, ushindi huo si kwa ajili ya Walebanoni peke yao, bali ni kwa ajili ya mataifa yote ya Waislamu wote duniani. Amefafanua kuwa, ushindi huo ulifikiwa kutokana na juhudi za kila aliyetoa mchango wake katika mapambano ya kuwang'oa Wazayuni nchini bali na si ushindi wa Hizbullah pekee. Hata hivyo yapo baadhi ya makundi nchini Lebanon, baada ya kushindwa kuipokonya silaha Harakati hiyo ya Hizbullah, sasa yanafanya njama nyingine za kuvunja kabisa harakati ya muqawama nchini humo. Vile vile amesema, hivi sasa Lebanon ina serikali dhaifu kiasi kwamba haiwezi hata kutatua mambo yake ya ndani kama vile kufikia mwafaka kuhusu sheria ya uchaguzi. Kwa mara nyingine amesisitiza kuwa, silaha za harakati ya muqawama zinatumika tu katika mapambano na Wazayuni na zitaendelea kupata uungaji mkono wa wananchi wa taifa hilo la Kiarabu. Aidha Katibu Mkuu wa Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya nchini Lebanon Hizbullah ameashiria kwamba, baadhi ya nchi zinafanya njama kubwa za kuliweka jina la harakati hiyo katika orodha ya makundi ya kigaidi na kusisitiza kuwa, njama hizo hazina taathira yoyote kwa Harakati ya Hizbullah. Amesema, suala la kuliweka jina la Hizbullah katika orodha ya makundi ya kigaidi duniani, itabakia kuwa wino tu juu ya karatasi, kwani harakati hiyo itaendelea na muqawama wake dhidi ya adui Mzayuni. Katika sehemu nyingine ya hotuba yake Sayyid Hassan Nasrullah ameashiria njama za baadhi ya mirengo ndani na nje ya Lebanon za kuvuruga hali ya usalama mjini Tripoli kaskazini mwa nchi hiyo na kusema kuwa, machafuko ya mjini Tripoli lazima yakomeshwe kwa thamani yoyote iwayo. Alisema jeshi la Lebanon pekee ndilo lenye dhamana ya kulinda usalama ndani ya nchi hiyo hususan katika keneo hilo. Aidha ameashiria hujuma za kila namna za mabeberu wanaopenda kujitanua wakiongozwa na Marekani wakishirikiana na baadhi ya tawala za kidikteta za Kiarabu pamoja na Uturuki dhidi ya taifa la Syria na kuzionya vikali nchi za eneo hili kutokana na hatari kubwa ya makundi ya Kiwahabi yenye misimamo mikali inayokufurisha Waislamu wengine. Katibu Mkuu wa Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya nchini Lebanon Hizbullah pia amesema, kile kinachojiri hivi sasa nchini Syria, ni matokeo ya uungaji mkono wa baadhi ya nchi za Kiarabu kwa makundi ya kigaidi. Alisema nchi hizo zinawatuma Mawahabi hao wenye misimamo mikali nchini Syria, ili zenyewe ziweze kuepukana na shari ya makundi hayo na wakati huo huo ziweze pia kuiangusha serikali halali ya Damascus. Sayyid Hassan Nasrullah amesema kama ninavyomnukuu: "Hivi sasa ulimwengu wa Kiislamu na Waislamu wako katika kipindi nyeti sana cha historia na haifai kupoteza muda kwani umefika wakati wa kusimama kidete kukabiliana na kimbunga hiki." Mwisho wa kunukuu. Amesema, machafuko ya nchini Syria ni kwa manufaa ya utawala haramu wa Kizayuni na ni hatari kubwa kwa nchi za eneo la Mashariki ya Kati na umma mzima wa Kiislamu.

No comments:

Post a Comment

TUPE MAWAZO YAKO