Saturday, May 04, 2013

MAPIGANO MAKALI YASHUHUDIWA NCHINI LIBYA


Mapigano makali yameshuhudiwa nchini Libya baada ya baadhi ya wananchi kuandamana wakipinga hatua ya wapiganaji kupiga kambi kwa takribani juma moja wakitaka kufukuzwa kazi kwa maofisa wote waliokuwa wakifanya kazi katika serikali ya Rais wa zamani wa nchi hiyo marehemu Kanali Muammar Ghaddafi. Mamia ya watu walikusanyika katika mji mkuu wa nchi hiyo Tripoli kupinga kitendo cha wapiganaji hao ambao wamejihami kwa silaha kuendelea kusalia nje ya majengo ya wizara ya mambo ya nje na ile ya sheria.
Hakuna taarifa za majeruhi wala kifo katika ghasia hizo ingawa kumekuwepo na taarifa za baadhi ya vikundi vya watu wenye silaha kuendelea kuwatishia waandamanaji wanaopingana nao katika miji mingine ya nchi hiyo ukiwamo ule wa mashariki wa Benghazi. Wapiganaji hao wengi wao ni wale walioshiriki mapambano yaliyofanikisha harakati za kumuondoa madarakani Kanali Ghaddafi aliyefariki dunia mnamo mwaka 2011. 
Serikali ya Libya imekuwa ikipitia pendekezo la sheria ya kuwaondoa Maofisa watu waliokuwa chini ya utawala wa Kanali Ghaddafi ambao bado wameendelea kusalia katika nyadhifa za juu.
Wachambuzi wa siasa za nchi hiyo wanaona kuwa iwapo pendekezo hilo litapitishwa na kuwa sheria litawaathiri wengi na kusababisha mifarakano na chuki kuendelea kukita mizizi katika Taifa hilo.

No comments:

Post a Comment

TUPE MAWAZO YAKO