Friday, May 31, 2013

WANACHAMA WA HAMAS NA FATAH WAKUTANA MISRI

Wawakilishi wa Harakati ya Muqawama wa Kiislamu ya Palestina HAMAS na wenzao wa Fat'h wamekutana katika mji mkuu wa Misri, Cairo kwa ajili ya duru nyengine ya mazungumzo, lengo likiwa ni kumaliza hitilafu zilizopo na kuleta umoja baina yao. Kwa mujibu wa Yahya Rabbah, afisa mwandamizi wa harakati ya Fat'h wajumbe wa harakati hiyo na wale wa Hamas walikutana hapo jana huko Cairo ili kufuatilia utekelezaji wa makubaliano ya kuleta maridhiano ya kitaifa kati ya Wapalestina. Rabbah amesisitiza juu ya kuundwa serikali ya umoja wa kitaifa na kuainishwa tarehe ya kufanyika uchaguzi bila ya masharti yoyote. Vikao vya viongozi wa Fat'h na Hamas vimekuwa vikifanyika katika kalibu ya kuendeleza mashauriano baina ya pande mbili kwa ajili ya kutekeleza makubaliano yaliyosainiwa huko nyuma hususan yale yanayohusiana na uundaji wa serikali ya umoja wa kitaifa na kuainishwa tarehe ya kufanyika uchaguzi huko Palestina. Mnamo mwezi Mei mwaka 2011 huko Cairo, Misri na Februari mwaka uliopita wa 2012 mjini Doha , Qatar, makundi ya Kipalestina yalitia saini hati za mwafaka wa kumaliza hitilafu na kuunda serikali ya umoja wa kitaifa. Hata hivyo hadi sasa mwafaka huo bado haujatekelezwa. Hamas ilishatangaza hapo kabla kuwa imelikubali wazo la kuundwa serikali ya umoja wa kitaifa ya Palestina itakayoongozwa na Rais wa Mamlaka ya Ndani Mahmoud Abbas na kwamba hivi sasa inasubiri jibu la harakati ya Fat'h. Safari ya hivi karibuni ya Mahmoud Abbas katika Ukanda wa Gaza iliyofanywa kwa lengo la kuleta umoja kati ya eneo hilo na lile la Ufukwe wa Magharibi ilipokewa kwa mikono miwili na viongozi wa Hamas; na hivi sasa Gaza inasubiri kwa hamu hatua muhimu inayopaswa kuchukuliwa na Rais wa Mamlaka ya Ndani ya kuunda serikali ya umoja wa kitaifa ili kufungua njia ya kufanyika chaguzi mbili muhimu za bunge la Palestina na Rais wa Mamlaka ya Ndani. Kwa mara ya mwisho uchaguzi wa Rais wa Mamlaka ya Ndani ulifanyika mwaka 2005 na ule wa bunge la Palestina ulifanyika mwaka 2006, na hivi sasa baada ya kupita miaka miwili tangu ulipomalizika muda ulioainishwa kisheria Wapalestina wanasubiri kufanyika uchaguzi mpya katika ardhi zao zinazokaliwa kwa mabavu. Kuundwa serikali ya umoja wa kitaifa sio tu kutaunganisha safu za Wapalestina bali kutawafungulia njia pia ya kuamua juu ya mustakabali wao wa kisiasa.
Ni wazi kwamba siasa za Marekani za kuchochea mifarakano ndizo zilizokwamisha juhudi za kuleta umoja baina ya Ukanda wa Gaza na Ufukwe wa Magharibi wa Mto Jordan. Kutenganishwa Gaza na Ufukwe wa Magharibi kulikofanikishwa kwa njama ya Marekani mnamo mwaka 2007 ndiko kulikozichonganisha harakati za Fat'h na Hamas na kuwadhoofisha Wapalestina katika kukabiliana na njama za utawala wa Kizayuni wa Israel. Utengano huo ndio uliorahisisha pia uendelezaji wa njama ya ujenzi wa vitongoji vya walowezi wa Kizayuni katika ardhi za Wapalestina. Katika mazingira kama hayo ambapo Marekani inafanya juu chini kuyafufua tena mazungumzo ya mapatano kati ya Wapalestina na utawala haramu wa Israel kwa gharama yoyote ile huku kukiwepo pia njama hatari za kuundwa eti nchi ya Palestina sambamba na dola la Kiyahudi lisilojumuisha Wapalestina ambao ni wakaazi wa ardhi za Palestina zilizoanza kukaliwa kwa mabavu mwaka 1948, ndipo viongozi wa Hamas wakasisitiza juu ya udharura wa Wapalestina kujihadhari na njama hizo na kuzidisha kasi ya harakati za kufanikisha mpango wa uundaji wa serikali ya umoja wa kitaifa ya Palestina

No comments:

Post a Comment

TUPE MAWAZO YAKO