Thursday, June 27, 2013

IRAN YAKAMATA MAJASUSI

Maafisa wa usalama wa taifa wa Iran wamefanikiwa kutambua na kusambaratisha mitandao hatari zaidi  ya ujasusi, ugaidi na uharibifu ambayo ilikuwa ikipata msaada wa mashirika ya ujasusi ya Marekani, utawala wa Kizayuni na baadhi ya nchi za eneo. Kwa mujibu wa Bw. Karimi, Mkurugenzi Mkuu wa Usalama wa Taifa katika mkoa wa Fars Kusini mwa Iran, mitandao hiyo ya kijasusi ilikuwa imepanga kutekeleza vitendo vya kikatili vya kigaidi kama vile kutega mabomu katika maeneo ya sala za Ijumaa, kushambulia maeneo ya kupiga kura na mikusanyiko ya wananchi katika siku za uchaguzi wa Juni 14. Bw. Karimi ameongeza kuwa maafisa wa usalama pia wamesambaratisha kundi linalofungamana na kijikundi cha kigaidi chenye misimamo mikali kinachopata himaya ya mashirika ya kijasusi ya nchi za Ulaya. Amesema kundi hilo lilikuwa limepanga pia kutekeleza hujuma za mabomu. Bw. Karimi ameendelea kusema kuwa maafisa wa usalama wa taifa pia wamewatambua na kuwatia mbaroni wanachama wa genge la kutayarisha na kusambaza silaha pamoja na zana za vita na kwamba genge hilo lilikuwa lina uhusiano na makundi yaliyo nje ya nchi. Amesema genge hilo pia lilikuwa linapanga kutekeleza hujuma wakati wa uchaguzi katika mkoa wa Fars, kusini mwa Iran.
Katika miaka ya hivi karibuni Iran imefanikiwa kusambaratisha makundi ya kijasusi na kigaidi yanayopata himaya ya mashirika ya kijasusi ya Marekani na utawala haramu wa Israel.

No comments:

Post a Comment

TUPE MAWAZO YAKO