Wednesday, June 26, 2013

UJERUMANI YATAKA MAJIBU YA UJASUSI WA UINGEREZA

Waziri wa sheria wa Ujerumani, Sabine Leutheusser-Schnarrenberger, amewaandikia barua mawaziri wawili wa Uingereza akitaka kupewa maelezo kamili kuhusu kiwango cha hatua za kijasusi za shirika la ujasusi la nchi hiyo ya Uingereza katika Ujerumani. Kwa mujibu wa gazeti la Guardian waziri huyo wa Ujerumani ametaka majibu kutoka Uingereza kuhusu mpango wa nchi hiyo unaojulikana kama Tempora uliotumiwa kuzichunguza data zote za mawasiliano za raia nchini Ujerumani. Mpango huo uliofichuliwa na mfichua siri wa Kimarekani Edward Snowden umewashtuwa wanasiasa mjini Berlin. Ujerumani imewataka mawaziri wa sheria na mambo ya ndani nchini Uingereza kufafanua juu ya uhalali wa mpango huo wa Tempora na nani aliyeuidhinisha. Wizara ya mambo ya ndani ya Uingereza imesema itajibu barua hiyo katika wakati mwafaka lakini haikutowa maelezo zaidi. Katika mpango huo wa kijasusi inadaiwa barua pepe, ujumbe katika mitandao ya kijamii, mawasiliano ya simu na nyendo nyinginezo kwenye mitandao za wakaazi wa Ujerumani zimekuwa zikifuatiliwa.

No comments:

Post a Comment

TUPE MAWAZO YAKO