Thursday, June 27, 2013

MURSI KUHUTUBIA TAIFA

Rais wa Misri, Mohammed Mursi, anajiandaa kulihutubia taifa kupitia televisheni hii leo. Hotuba ya rais huyo inatazamiwa kutowa mwelekeo wa hatma yake kisiasa wakati mamilioni ya watu wa nchi hiyo wakijiandaa mwishoni mwa wiki hii kwa maandamano ya kumtaka aondoke madarakani. Inaarifiwa kwamba hofu za kuzuka vurugu kati ya wafuasi wa rais huyo na wapinzani wao kutoka vyama mbalimbali walioungana imewafanya wakaazi kununua vyakula na mafuta kwa wingi kuepuka adha itakayosababishwa na vurugu hizo. Jeshi pamoja na polisi wanajiandaa kukabiliana na hali yoyote ya vurugu itakayojitokeza. Tayari polisi imeongeza vifaa na askari katika maeneo kadhaa ya majengo muhimu ya serikali. Hotuba ya Mursi haijafahamika itazungumzia kitu gani lakini wasaidizi wake wameitaja hotuba hiyo kuwa muhimu kabisa. Baadhi wanahisi huenda akafanya mageuzi makubwa katika baraza lake la mawaziri ili kujaribu kuzimaliza hasira za wapinzani dhidi yake.

No comments:

Post a Comment

TUPE MAWAZO YAKO