Tuesday, June 11, 2013

RUSSIA YASEMA WAASI WA SYRIA WANATUMIA SILAHA NZITO

Waziri wa Mambo ya Nje wa Russia amesema kuwa, waasi nchini Syria wanatumia silaha nzito katika mashambulizi yao. Sergei Lavrov amesema waasi wanaopigana dhidi ya serikali ya Damascus, walitumia silaha nzito ikiwemo mizinga na silaha nyingine za anga katika mapigano makali na jeshi la nchi hiyo kwenye mji uliokombolewa na serikali wa al-Qusair. Lavrov ameyasema hayo alipokuwa akizungumza na televisheni ya CBS na kusisitiza kuwa, waasi hao ni hatari kubwa kwa usalama wa dunia. Seneta wa chama cha Republicans cha nchini Marekani, John McCain ambaye hivi karibuni aliingia kinyemela nchini Syria, kwa mara kadhaa amekuwa akiitaka serikali ya Washington kuingia kijeshi nchini humo na kuwapatia silaha nzito waasi wa Syria. Seneta huyo mwenye misimamo ya kufurutu mipaka amesisitiza kuwa, waasi wa Syria, wanahitaji sana silaha nzito ili waweze kukabiliana na jeshi la nchi hiyo, linaloelekea kushinda vita vyake dhidi ya makundi ya waasi.  

No comments:

Post a Comment

TUPE MAWAZO YAKO