Serikali ya Mali na waasi wa Tuareg wamekubaliana kuhusu kufanyika kwa uchaguzi Mkuu wa mwezi ujao katika eneo la Kidal ambalo kundi hilo linathibiti. Maafikiano hayo yalifikiwa siku ya Jumatatu jijini Ouagadougou, nchini Burkinafaso baada ya siku tatu ya mazungumzo kati ya pande hizo mbili muda mfupi baada ya majeshi ya serikali kuanza oparesheni dhidi ya kundi lingine la waasi la MNLA .
Kundi la MNLA limekataa wito wa serikali ya Mali kurudisha silaha na linapinga kuja kwa majeshi ya serikali jijini Kidal. Serikali ya Bamako imekuwa ikisema inataka uongozi wake katika eneo la Kidal kabla ya Uchaguzi Mkuu wa tarehe 28 mwezi ujao na kutishia kuchukua mji huo ikiwa suluhu halingepatikana.
Kundi la Tuareg kwa muda mrefu limekuwa likitaka kujitenga na kujiongoza kivyao na wanaliita Azawad kwa madai kuwa eneo hilo limekuwa likitengwa kimaendeleo na kisiasa na uongozi wa Bamako. Baada ya mapinduzi ya serikali kutokea nchini humo mwaka uliopita, kundi la Turaeg liliungana na makundi mengine ya Kislamu kujitenga na serikali ya Bamako na kuzua ukosefu wa usalama Kaskazini mwa nchi hiyo suala ambalo lilisababisha Ufaransa kuzindua Oparesheni ya kijeshi dhidi ya waasi hao . Serikali ya Ufaransa imesema kuwa itawaachia jukumu la kulinda amani jeshi la Umoja wa Mataifa mwezi ujao baada ya kuwa nchini humo kuanzia mapema mwaka huu.
No comments:
Post a Comment
TUPE MAWAZO YAKO