Tuesday, June 25, 2013

UHUSIANO WA RUSSIA NA MAREKANI WAZIDI KUKOROGEKA

Uhusiano kati ya Russia na Marekani umezidi kuvurugika baada ya Moscow kushindwa kumkamata afisa wa zamani wa CIA aliyeanika hadharani siri za Washington wiki mbili zilizopita. Edward Snowden, hivi majuzi alifichua kwamba Marekani imekuwa ikidukua mitandao ya intaneti kama vile Google, Facecook, Youtube na Yahoo na kukusanya taarifa za siri za watu kote duniani; jambo ambalo ni kinyume na sheria za kimataifa. Snowden pia alifichua kwamba mashirika ya kijasusi ya Marekani ya CIA na NSA yamekuwa yakinasa mazungumzo ya simu ya watu kote duniani. Ufichuzi huo uliamsha hasira za watu hususan huko Marekani ambako katiba ya nchi imesisitiza kuheshimiwa faragha ya mtu. Snowden alikimbilia Hongkong baada ya ufichuzi huo na hapo jana aliondoka na kuelekea Russia akiwa njiani kwenda Ecuador. Washington ilikuwa imeiomba Moscow kumkamata afisa huyo wa zamani wa CIA na kumrudisha nyumbani lakini hilo halikufanyika. Kwa sasa Snowden ameelekea Ecuador anakotarajiwa kupata hifadhi ya kisiasa. Wachambuzi wa mambo wanasema kwa kuzingatia jinsi mgogoro wa Syria ulivyozigawa Marekani na Russia, kadhia ya Snowden inatarajiwa kupanua zaidi ufa wa kidiplomasia ulioko kati ya nchi mbili hizo.

No comments:

Post a Comment

TUPE MAWAZO YAKO