Wednesday, July 24, 2013

IRAN YAPINGA HIZBULLAH KUINGIZWA KATIKA LIST YA MAGAIDI

Serikali ya Iran imepinga vikali hatua ya Umoja wa Ulaya EU kuliorodhesha Kundi la Wanamgambo wa Hezbollah katika orodha ndefu ya Makundi ya Kigaidi Duniani wakisema hatua hiyo imechangiwa na shinikizo na kuangalia maslahi ya nchi ya Israel. Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran Ali Akbar Salehi amelaani uamuzi huo wa Umoja wa Ulaya EU ambao umepata ushawishi kutoka kwa Taifa hilo la Kiyahudi ambalo limekuwa likishinikiza Kundi la Hezbollah kutambulika kama moja ya makundi ya kigaidi. Salehi amesisitiza kuwa Umoja wa Ulaya EU umekosa pakubwa kwenye uamuzi wake na hilo linachangiwa kwa kiasi kikubwa kutokana na wao kukosa taarifa muhimu juu ya mgogoro unaoendelea kwenye kanda hiyo.
Waziri huyo mwenye dhamana ya masuala ya kigeni katika Serikali ya Tehran amesema Kundi la Wanamgambo wa Hezbollah tangu lililopokuwa litatambulika kihalali limeweza kuwalinda wananchi wa Lebanon dhidi ya hila za taifa la Israel. Taifa la Iran na Kundi la Wanamgambo wa Hezbollah wamejiapiza mara zote kuwa Israel ni adui yao na wapo tayari kufanya hata mashambulizi kulilenga Taifa hilo ili waliangamize kitu ambacho kilichangia Serikali Jerusalem kutaka kuwekewa vikwazo kwa Kundi hilo. Serikali ya Iran nimiongoni mwa vyanzo vikubwa vya mapato vya Kundi la Wanamgambo wa Hezbollah huku pia ikiweka bayana wamekuwa wakitoa msaada wa kijeshi kuhakikisha linaendelea na shughuli zake.
Uamuzi huo wa nchi wanachama ishirini na nane za Umoja wa Ulaya EU umeungwa mkono na Baraza la Taifa la Upinzani nchini Syria ambalo limesema ni sahihi kutokana na Hezbollah kuwa hatari kwenye Ukanda huo. Baraza la Taifa la Upinzani nchini Syria limeweka bayana uamuzi huo wa Umoja wa Ulaya EU usiishie hapo na badala yake Viongozi wa Kundi la Wanamgambo wa Hezbollah wanapaswa kufunguliwa mashtaka ya uhalifu wa vita. Wapinzani nchini Syria wamesema kitendo cha Kundi la Hezbollah kuingilia vita nchini Syria na kulisaidia Jeshi la Rais Bashar Al Assad ni kigezo kingine kuonesha namna ambavyo limekuwa hatari kwa usalama.

No comments:

Post a Comment

TUPE MAWAZO YAKO