Dzhokhar Tsarnaev anayetuhumiwa kuhusika na mlipuko wa bomu katika mji wa Boston amekana tuhuma za kuhusika na mlipuko huo. Kijana huyo mwenye umri wa miaka 19 na mwenye asili ya Chechnia ameiambia mahakama inayoshughulikia kesi hiyo kamba hakuhusika kwa njia yoyote na mlipuko wa bomu uliotokea wakati wa mbio za Marathon katika mji wa Boston. Tsarnaev alitiwa nguvuni na polisi ya Marekani siku mbili baada ya mlipuko huo uliosababisha vifo vya watu watatu. Dzhokhar Tsarnaev anakabiliwa na tuhuma 30, na hukumu ya 17 kati ya tuhuma hizo ni adhabu ya kifo au kifungo cha maisha jela. Kwa mujibu wa mashtaka yaliyotayarishwa na vyombo vya usalama na mahakama za Marekani Tsarnaev anakabiliwa na hatima mbaya. Kwani itakuwa vigumu mno kuweza kujinasua na tuhuma 30 ambazo adhabu ya nyingi kati yazo ni hukumu ya kifo. Ripoti zinasema kuwa, baada tu ya kutiwa nguvuni, Dzhokhar Tsarnaev alisailiwa vikali na vyombo vya upelelezi vya Marekani. Inasemekana pia kwamba, wakati mwingine alikuwa akisailiwa kwa kipindi cha masaa 16 bila hata ya kuheshimiwa haki zake za kimsingi. Ripoti zinasema kuwa maafisa wa upelelezi wa Marekani waliwazuia hata mawakili wa kijana huyo mwenye umri wa miaka 19 kuhudhuria vikao vya kumsaili.
Tukiachia mbali suala la hatima inayomsubiri Dzhokhar Tsarnaev, kwa sasa fikra za waliowengi nchini Marekani zinataka kupata majibu ya maswali kwamba, Tsarnaev na kaka yake aliyeuliwa na jeshi la Marekani Tamerlan Tsarnaev, walikuwa peke yao katika kutega bomu hilo, au walipata msaada wa watu wengine? Wamarekani wanataka kujua ni kwa nini vyombo vya usalama vya nchi hiyo havikuweza kuzuia mlipuko wa Boston licha ya kuwepo jina la Tamerlan Tsarnaev katika orodha ya watu wanaodhaniwa kuwa ni magaidi? Je, Tamerlan Tsarnaev aliwahi kushirikiana na vyombo vya upelelezi vya Marekani au la? Na je maafisa wa polisi ya federali FBI wangeweza kumkamata Tamerlan akiwa hai, au hawakuwa na budi isipokuwa kumpiga risasi na kumuua?
Kwa kutilia maanani mwenendo mrefu wa kesi kama hizi nchini Marekani, inaonekana kuwa majibu ya maswali haya hayawezi kupatikana katika kipindi cha siku au hata wiki kadhaa zijazo. Pamoja na hayo weledi wa mambo wanasema kuwa hata mwisho wa kesi hii hautafichua ukweli wa mambo kuhusu hakika ya mlipuko wa bomu wakati wa mashindano ya Marathon mjini Boston. Wachambuzi hao wanafananisha kesi hii na ile ya matukio ya Septemba 11 mwaka 2001 ambayo sehemu moja ya matokeo ya uchunguzi wake imebakia kuwa siri ya hali ya juu ambayo hata wananchi wa Marekani hawaruhusiwi kujua undani wake.
No comments:
Post a Comment
TUPE MAWAZO YAKO