Maana ya kufunga (Swawm) ni kujizuilia. Neno Swawm kwa maana ya kujizuilia linaweza kutumika katika kujizuia kufanya jambo lolote la kawaida mtu alilozoea kulifanya. Katika Qur-aan tunafahamishwa kuwa Bibi Maryam baada ya kumzaa Nabii ‘Iysaa (‘Alayhis Salaam) alijizuia (alifunga) ili asiseme na mtu neno lolote juu ya mtoto wake. “...Na kama ukimwona mtu yoyote (akauliza habari za mtoto huyu) sema: Hakika mimi nimeweka nadhiri kwa Mwingi wa Rehema ya kufunga, kwa hiyo leo sitasema na mtu.” (19: 26). Katika Uislamu kufunga (Swawm) ni kujizuilia kula, kunywa, kuvuta sigara, kuingiza kitu chochote katika matundu mengine mawili kama vile pua na masikio, kujizuia na kujamii, kujitoa manii kwa makusudi au kwa matamanio na kujizuia kujitapisha kwa ajili ya Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala), kwa kipindi cha kati ya Al-fajri ya kweli mpaka kuingia magharibi. Hii ndio maana ya nje ya Swawm katika Uislamu.
Kufunga katika Uislamu kuna maana ya ndani zaidi, ambayo kama haikufikiwa, kuzuilia kufanya vitendo hivyo vilivyoelezwa hakutakuwa na maana yoyote kwa mfungaji. Kufunga kwa maana ya ndani ni pamoja kujizuilia kutenda maovu yote yaliyokatazwa na Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala). Ili Swawm ya mfungaji iwe na maana na yenye kufikia lengo, hana budi kukizuilia (kukifungisha) kila kiungo chake cha mwili - macho, ulimi, masikio, mikono na miguu- pamoja na fikra na hisia zake na matendo aliyokataza Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala). Funga ya macho ni kujizuilia na kuangalia aliyoyakataza Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala); Funga ya ulimi ni kujizuilia na mazungumzo yote aliyoyakataza Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) kama vile kusengenya, kusema uwongo, kugombana na kadhalika, funga ya masikio ni kujizuia kufanya yale yote aliyoyaharamisha Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala); funga ya miguu ni kujizuilia na kuendea yale yote aliyoyakataza Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) funga ya fikra na hisia ni kujizuia na fikra na dhana mbaya ambazo zinampelekea kuvunja amri na makatazo ya Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala). Ni katika maana hii Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam)anasema katika Hadithi zifuatazo:
No comments:
Post a Comment
TUPE MAWAZO YAKO