Saturday, July 20, 2013

SERIKALI YA NDANI YA PALESTINA YASALITI WAPALESTINA

Duru za habari zimetangaza kuwa Mamlaka ya Ndani ya Palestina imekubali kuendelea na mazungumzo eti ya amani ya Mashariki ya Kati licha ya upinzani wa Wapalestina na sisitizo la Mamlaka hiyo kuwa haitafanya mazungumzo ya aina yoyote na Wazayuni kutokana na ujenzi wake wa vitongoji vya walowezi wa Kiyahudi katika ardhi za Palestina.   Pamoja na kuwa hakuna taarifa zaidi zilizotolewa kuhusu makubaliano ya Wapalestina na utawala za Kizayuni kwa ajili ya kuanzisha tena duru mpya ya mazungumzo eti ya mapatano, lakini Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Marekani John Kerry alisema jana usiku baada ya kuhitimisha safari yake ya sita katika eneo la Mashariki ya Kati baada ya kuchukua wadhifa wake huo kuwa, pande husika zitaanza kufuatilia duru mpya ya mazungumzo ya mapatano huko Washington katika wiki ijao.
Mazungumzo ya moja kwa moja kati ya utawala wa Kizayuni wa Israel na Serikali ya Ndani ya Palestina yalisimama mwezi Oktoba mwaka 2010, wiki nne tu baada ya kuanza huko Washington. Mazungumzo hayo yalisitishwa baada ya utawala wa Kizayuni kukataa kusitisha ujenzi wa vitongoji vya walowezi wa Kiyahudi katika Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan na Baitul Muqaddas ya Mashariki. Japokuwa hatua ya Serikali ya Ndani ya Palestina ya kukubali kuanzisha tena duru mpya ya mazungumzo chini ya mashinikizo ya Marekani imekaribishwa na Catherine Ashton, Mkuu wa Siasa za Nje wa Umoja wa Ulaya na utawala wa Kizayuni, lakini makundi ya Kipalestina hususan harakati ya Hamas, Jihadul Islami na Harakati ya Ukombozi wa Palestina zimepinga kuanza tena mazungumzo hayo eti ya mapatano na kusisitiza kuwa, Mahmoud Abbas hana mamkala ya kuwa msimamizi na mzungumzaji wa masuala muhimu yanayowahusu Wapalestina.  Hii ni kwa sababu kipi cha kisheria cha urais wa Abbas kilimalizika miaka kadhaa iliyopita. Wananchi na makundi ya Kipalestina yanaona kuwa kurejea kwenye meza ya mazungumzo na Israel bila ya kuzingatia maazimio ya Umoja wa Mataifa ni sawa na kuwauwa kisiasa Wapalestina na kutoa mwanya kwa utawala ghasibu wa Israel wa kutenda jinai zaidi dhidi ya Wapalestina.
Wakati huo huo Avigdor Lieberman waziri wa zamani wa mambo ya nje wa utawala wa Kizayuni amesema kuwa Tel Aviv kamwe haipo tayari kuanzisha tena mazungumzo ya mapatano na serikali ya Ndani ya Palestina kuhusu mipaka ya mwaka 1967. Lieberman ameyatamka hayo katika radiamali yake kwa habari zilizochapishwa kwamba Israel imekubali kufanya mazungumzo na Mamlaka ya Ndani ya Palestina katika fremu ya mipaka iliyoghusubiwa mwaka 1967. Msimamo huo unaonyesha kuwa utawala wa Kizayuni ungali unang'ang'ania takwa lake la kuendelea kughusubu maeneo ya Palestina. Duru mpya ya jitihada za Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Marekani za kufufua mazungumzo eti ya mapatano inakamilika huku raia wengi na makundi ya Kipalestina wakiyataja mazungumzo hayo kuwa yatakuwa na madhara kwa malengo ya muda mrefu ya wananchi wa Palestina.
Alaa kulli hal, kama ilivyosemwa mara kadhaa ni kuwa lengo la safari za kila mara za viongozi wa Marekani katika eneo la Mashariki ya Kati ni kuzipotosha fikra za walio wengi ili kuficha mipango haramu ya ujenzi wa vitongoji vya walowezi inayofanywa na utawala wa Kizayuni sambamba na kukanyaga haki za wananchi wa Palestina kupitia mipango hiyo ya urongo.  

No comments:

Post a Comment

TUPE MAWAZO YAKO