Sunday, July 28, 2013

SHAMBULIZI LA MAREKANI LAUA 60 AFGHANISTAN

Watu wasiopungua 60 wameuliwa katika mashambulio tofauti ya anga yaliyofanywa na vikosi vya majeshi ya kigeni yanayoongozwa na Marekani katika mikoa ya Paktia, Kunar na Helmand nchini Afghanistan. Watu wasiopungua 45 waliuliwa hapo jana wakati majeshi ya kigeni yalipofanya mashambulio ya anga katika mkoa wa Helmand ulioko kusini mwa Afghanistan. Majeshi hayo yanayoongozwa na Marekani yamezidisha mashambulio ya anga katika maeneo ya raia nchini Afghanistan katika miezi ya hivi karibuni. Vifo vya raia vinavyotokana na mashambulio ya anga yakiwemo ya ndege zisizo na rubani za Marekani vimekuwa chanzo cha misuguano kati ya serikali ya Afghanistan na vikosi vya majeshi ya kigeni yanayoongozwa na Marekani na kuzidisha pia chuki dhidi ya Washington nchini Afghanistan. Marekani na waitifaki wake waliivamia Afghanistan mwaka 2001 ikiwa ni katika sehemu ya kile kilichotajwa kuwa vita dhidi ya ugaidi. Licha ya kuiondoa madarakani serikali ya kundi la Taliban, machafuko na umwagaji damu unaendelea kushuhudiwa nchini Afghanistan tangu wakati huo hadi sasa pamoja na kuweko maelfu ya askari wa majeshi ya kigeni yanayoongozwa na Marekani

No comments:

Post a Comment

TUPE MAWAZO YAKO