Sunday, December 30, 2012

JESHI LA MAJINI LA IRAN LAENDELEA NA MAZOEZI MAKALIA


Jeshi la Wanamaji la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran linaendeleza mazoezi makubwa ya kijeshi ambapo ndege zisizo na rubani pamoja na ndege za upelelezi na helikopta zimetumika katika luteka hiyo. Akizungumza na Shirika la Habari la Fars, Admeli Amir Rastegari ambaye ni msemaji wa maneva hiyo ameongeza Jumamosi ilikuwa siku ya pili ya mazoezi hayo ambapo jeshi la wanamaji lilionyesha mbinu zake katika kukabiliana na adui baharini. Mazoezi hayo ya Jeshi la Wanamaji la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran yaliyopewa jina la ‘Wilayat 91’ yalianza Ijumaa na yataendelea kwa muda wa wiki moja.  Luteka hiyo itafanyika katika eneo lenye ukubwa wa kilomita mraba milioni 1 kutoka Ghuba ya Uajemi hadi Bahari ya Hindi na Ghuba ya Aden. Mazoezi hayo yanajumuisha nyambizi, manoari, makombora, ndege zisizo na rubani na vita vya kielektroniki.

WAANDAMANAJI BAHRAIN WAZIDI KUKANDAMIZWA


Viongozi wa kisiasa nchini Bahrain wameukosoa vikali utawala wa kifalme wa Aal Khalifa kwa kufanya njama dhidi ya wafanya mapinduzi nchini humo. Wapinzani Bahrain wameongeza kuwa, katika kujaribu kuzima wimbi la mwamko wa wananchi utawala wa dhalimu wa ukoo wa Aal Khalifa unatumia mbinu za hadaa na ukandamizaji. Abdullah Al-Gharifi aliyasema hayo hapo jana kupitia televisheni ya Al-Lu'uluat na kusisiza kuwa, katika kuzipotosha fikra za walio wengi na kuyapindisha malengo halali ya Mwamko wa Kiislamu wa wananchi, utawala wa Aal Khalifa umeanzisha wimbi jipya la njama kadhaa.  Amesema sasa wananchi wote wamefahamu hila za utawala huo na kwamba, malengo ya mapinduzi yanakaribia. Kiongozi huyo amesisitiza kuwa,  pamoja na njama hizo na ukandamizaji unaofanywa na askari wa utawala huo kwa kushirikiana na askari vamizi wa Saudia, bado wananchi wameendelea kusimama imara kwa ajili ya kufikia malengo yao.


WAPALESTINA WASHAMBULIWA NA HOMA YA H1N1


Kwa akali Wapalestina 9 wamefariki dunia kutokana na kukumbwa na aina ya kutisha ya homa ya H1N1 katika Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan huko katika ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu. Hapo jana viongozi wa Palestina walitangaza kuwa, Wapalestina hao walifariki dunia katika kipindi cha wiki mbili zilizopita baada ya kukumbwa na homa ya H1N1. Viongozi hao wamesisitiza kuwa, hadi sasa Wapalestina wengine wapatao 189 wameathirika na homa hiyo katika eneo hilo la Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan. Viongozi wa Palestina pia wametangaza kuwa, tayari Shirika la Afya la Umoja wa Mataifa WHO limekubali kutuma chanjo kwa ajili ya kukabiliana na homa ya H1N1.

Yaa rabbi wape shifaa yako ndugu zetu hawa na uwape nguvu ya kuitetea nchi yao na uislam kwa ujumla AAMin

MAREKANI SUALA LA FEDHA BADO TATA


Duru za habari kutoka Marekani zinaarifu kuwa, viongozi wa kisiasa wa vyama vya Republican na Democrats wameendelea kulumbana kutokana na kushadidi kwa hali mbaya ya uchumi wa nchi hiyo. Sintofahamu hiyo imetokea kuhusiana na juu ya namna gani ya kutatua matatizo hayo ya kiuchumi ili kuweza kuwapunguzia wananchi wa nchi hiyo mzigo wa mgogoro wa kiuchumi. Mkuu wa taasisi ya Centre for Corporate Policy iliyopo mjini Washington Bwana Charlie Cray amesema kuwa, jamii ya watu wa tabaka la kati nchini Marekani, ndio wahanga wa malumbano ya kisiasa nchini humo. Ameongeza  kuwa, hali hiyo imezidisha ongezeko la ukosefu wa ajira na mgogoro wa kiuchumi. Mtaalamu huyo wa masuala ya kiuchumi pia amesisitiza kuwa, hali mbaya zaidi inawakabili Wamarekani wenye asili ya Kiafrika na kwamba kiwango cha ukosefu wa ajira katika tabaka hilo kimefikia asilimia 12.4, ambapo wengi wao ni vijana walio na umri wa kati ya miaka 18 hadi 29.

WAZAYUNI WAZIDI KUANDAMANA


Jinamizi la maandamano na migomo linazidi kuusakama utawala wa Kizayuni wa Israel huku mwaka huu wa 2012 ukielekea ukingoni. Matukio ya huko Palestina inayokaliwa kwa mabavu na Wazayuni yanabainisha kwamba, Israel itaingia katika mwaka mpya wa 2013 huku ikiandamwa na wimbi la maandamano na malalamiko ya Wazayuni kutokana na kushadidi mgogoro wa kiuchumi na kile kinachoonekana kuwa, kutokuwa na ustahiki na uwezo viongozi wa Tel Aviv wa kutatua migogoro lukuki inayoukabili utawala huo haramu. Kupanuka wigo wa malalamiko, migomo na maandamano huko Palestina inayokaliwa kwa mabavu kunatokea katika hali ambayo, sekta mbalimbali za kiuchumi za Israel nazo zimo katika hali ya kufilisika huku wafanyakazi wengi wakikabiliwa na hatari ya kukosa ajira zao. Katika fremu hiyo mamia ya wafanyakazi wa shirika kubwa kabisa la simu la Israel la Pelephone wameandamana mjini Tel Aviv na kukusanyika mbele ya nyumba ya Gil Sharon, mkurugenzi mtendaji wa shirika hilo. Mgomo wa wafanyakazi wa shirika hilo la simu umeingia katika wiki yake ya nne. Hii ni katika hali ambayo, wafanyakazi wa Bezeq shirika jengine linalotoa huduma za simu, wamejiunga na wenzao wa Pelephone katika mgomo huo. Kujiunga wafanyakazi wa mashirika hayo ya simu na mgomo wa wafanyakazi wa mashirika mengine, kumeifanya migomo dhidi ya Israel iingie katika hatua na marhala mpya kabisa.  Gazeti la Israel la Haaretz limeripoti juu ya kuenea mgomo na maandamano ya wafanyakazi wa kiwanda cha ufumaji cha utawala huo ghasibu. Kwa mujibu wa ripoti hiyo waandamanaji hao wakiwa na mabango na maberamu wamechoma matairi na kufunga njia ya mlango mkuu wa kiwanda hicho kwa kuweka mkusanyiko mkubwa. Hii ni katika hali ambayo, wafanyakazi wa viwanja vya ndege vya Israel nao wametishia kuwa, endapo hawatoongezewa mishahara na kuboroshewa huduma na suhula za kazi watafanya mgomo katika kipindi hiki cha kukaribia mwaka mpya wa Miladia. Shirika la Umeme la Israel ambalo ndilo shirika pekee la umma linalotoa huduma ya ugavi wa umeme huko Palestina inayokaliwa kwa mabavu limetangaza kuwa, linakaribia kukabiliwa na matatizo makubwa ya kifedha kutokana na mzigo mkubwa wa madeni; hivyo huenda likawafukuza kazi wafanyakazi wake 2000 waliojiriwa rasmi. Kwa hakika kushadidi mgogoro wa kiuchumi wa utawala wa Kizayuni wa Israel kunabainisha kugonga ukuta hatua za viongozi wa Israel za mwaka huu wa 2012 za kumfukuza pepo mbaya wa mgogoro wa kiuchumi wa utawala huo ghasibu. Kwa mukatadha huo, mwaka huu wa 2012 unaweza kupewa jina la “mwaka  wa kushadidi migogoro mbalimbali ndani ya utawala wa Kizayuni wa Israel” ikiwemo ya kisiasa, kiuchumi na kijamii. Kama vile haitoshi, takwimu mbalimbali zinaonesha kuwa, katika mwaka huu wa 2012 vitendo vya jinai na uhalifu vimeongezeka sana huko Israel. Fauka ya hayo, kushikana mashati, kunyoosheana vidole vya lawama na mivutano ya kisiasa nayo imeonekana kushika kasi baina ya viongozi wa utawala huo; jambo ambalo limeifikisha Israel katika hatua ya kufanyika uchaguzi wa Bunge wa kabla ya wakati ambao unatarajiwa kufanyika Januari 22 mwakani. Ala kulli haal, mwenendo wa kuongezeka migogoro ya kiuchumi, kisiasa na kijamii huko Israel ni jambo linalobainisha kwamba, kivitendo viongozi wa utawala huo hawana ubavu wa kudhibiti hali ya mambo na kwamba harakati ya utawala huo inaelekea upande wa kuangamia na kusambaratika. Wachambuzi wa mambo wanaamini kwamba, kukithiri malamamiko na maandanao ya raia wa Kizayuni ni ithbati tosha kuwa, Israel sio tu kwamba, haina uhalali kimataifa, bali haikubaliki hata na raia wake wenyewe; na kwa msingi huo hatima ya utawala kama huu si nyingine ghairi ya kuangamia na kusambaratika.

WAPALESTINA YAIKOSOA MAREKANI

Mamlaka ya Ndani ya Palestina imeikosoa Marekani kwa kuwashinikiza Mawaziri wa Mambo ya Nje wa nchi za Kiarabu wasimamishe safari yao ya kutembelea Ukingo wa Magharibi wa Mato Jordan. Ukosoaji huo umetolewa baada ya Mawaziri wa Mambo ya Nje wa nchi 4 za Kiarabu kukataa kuandamana na Waziri Mkuu wa Jumuiya ya Nchi za Kiarabu Nabil al Arabi katika safari yake ya kwanza ya kutembelea Ramallah. Wasel Abu Yussuf afisa wa ngazi za juu wa Harakati ya Ukombozi wa Palestina (PLO) amesema, Wamarekani wamewazuia mawaziri hao wa Kiarabu kutembelea Ramallah na kwamba Marekani na Israel zilizitaka nchi za Kiarabu kuwawekea vikwazo vya kifedha Wapalestina katika Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan baada ya kupigwa kura ya kutambuliwa Palestina kama nchi isiyokuwa mwanachama katika Umoja wa Mataifa mwezi uliopita. Al Arabii aliyetembelea Ramallah ili kujadili matatizo ya kifedha yanayoikabili Palestina, alirejea nyumbani haraka baada ya kuahidi kuisaidia Mamlaka ya Ndani ya Palestina.

Saturday, December 29, 2012

IRAQ YAKABILIWA NA WIMBI LA NJAMA MPYA

Matukio ya siku chache zilizopita nchini Iraq yamefichua njama mpya zinazopangwa na pande kadhaa dhidi ya nchi hiyo.
Ijumaa ya jana tarehe 28 Disemba miji ya al Anbar, Salahuddin na Mosul ilikumbwa na maandamano ya wapinzani wa serikali ya sasa ya Baghdad. Waandamanaji hao waliojumuisha wafuasi wa chama tawala zamani cha Baath walibeba bendera ya utawala wa zamani wa Iraq na ya makundi ya wapinzani wa serikali ya Syria huku wakipiga nara dhidi ya serikali ya Iraq. Wakati huo huo na sambamba na maandamano hayo, habari zinasema kuwa chama cha dikteta wa zamani wa Iraq Saddam Hussein cha Baath kimezindua televisheni iliyopewa jina la Falluja kwa msaada wa kifedha wa Qatar. Vilevile kuna habari kwamba kumeanzishwa kundi la wanamgambo lililopewa jina la Jeshi la Ukombozi wa Iraq chini ya uongozi wa Izzat Ibrahim Al Douri, aliyekuwa makamu wa dikteta aliyenyongwa wa Iraq kwa ajili ya kuratibu tena harakati za wafuasi wachama cha Baath nchini humo. Matukio haya yote hayatokei kwa sadfa na yanafichua kwamba kuna sinario na njama inayotekelezwa kwa mpangilio maalumu dhidi ya Iraq.
Baadhi ya weledi wa masuala ya kisiasa wanaamini kuwa, matukio ya sasa katika eneo la Mashariki ya Kati hususan hali tata iliyojitokeza huko Syria na vilevile hitilafu zilizoibuka kati ya Wakurdi na serikali ya Baghdad vimetayarisha mazingira kwa makundi ya kichochezi ya ndani na nchi za kigeni kuingilia masuala ya Iraq na kuanza kusambaza sumu na fitina dhidi ya serikali ya Baghdad. Hasa ikitiliwa maanani kwamba shakhsia mkubwa kama Jalal Talabani, Rais wa Iraq ambaye anaaminiwa na karibu makundi yote nchini humo na daima amekuwa mstari wa mbele katika kutatua hitilafu za ndani, amelazwa hospitani akiwa taabani.
Katika hali kama hiyo inaonekana kuwa Magharibi na nchi za Kiarabu zinazofuata sera za Marekani kama Saudi Arabia, Qatar na Uturuki zimezidisha fitina na mchezo mchafu wa kueneza hitilafu ndani ya Iraq. Hii ni pamoja na kuwa, Marekani bado inafanyia kazi mpango wa kuzigawa baadhi ya nchi za Mashariki ya Kati hususan Iraq.
Marekani na waitifaki wake wa Kiarabu wanatumia mbinu ya kuzusha machafuko ya kimadhehebu na kikaumu katika baadhi ya nchi za Mashariki ya Kati kama Lebanon, Syria na Iraq. Baada ya kuzusha mapigano ya kikaumu na kimadhehebu huko kaskazini mwa Lebanon na vita vya ndani huko Syria inaonekama kuwa sasa imewadia zamu ya Iraq.
Wachambuzi wa mambo wanasema kuwa, moto wa hitilafu zilizotokea kati ya viongozi wa eneo la Kurdistan na serikali ya Baghdad na kuyalazimisha majeshi ya pande hizo mbili kuelekezeana mitutu ya bunduki, na maandamano yaliyofanyika kwa lengo la kuchochea hitilafu za kimadhehebu kati ya Waislamu wa Kishia na Kisuni katika maeneo ya Wasuni wengi umewashwa na nchi za kigeni na ni ishara kuwa Iraq inakabiliwa na njama na tishio kubwa.
Ni kwa sababu hiyo ndiyo maana Waziri Mkuu wa Iraq Nuri Al Maliki akasema waziwazi kuwa, sera za kuzusha hitilafu za kimadhehebu na kikaumu hazitaifikisha popote Iraq na ameyaasa makundi yote ya upinzani kuketi kwenye meza ya mazungumzo.      

HAKUNA MWENYE UWEZO WA KUIZUIA IRAN


Rais Mahmoud Ahmadinejad amesema kuwa, maadui hawana ubavu wa kuzuia harakati ya maendeleo na ustawi wa taifa la Iran. Dakta Ahmadinejad amezikosoa siasa za kindumakuwili pamoja na njama za maadui dhidi ya Iran na kusisitiza kuwa, taifa hili litaendelea kufanya harakati kuelekea ustawi na maendeleo na kwamba, maadui hawana ubavu wa kuzuia harakati hii.
Rais Ahmadinejad amesema, nguvu na uwezo wa taifa la Iran utashinda muamala mbaya wa maadui wa taifa hili. Ahmadinejad ameongeza kuwa, maadui wamekuwa wakiongea na taifa hili kwa lugha chafu na isiyo na adabu na kwamba, ukosefu wao huo wa adabu kwa taifa hili utawafanya maadui hao wajute. Amesema bayana kwamba, ni zaidi ya miaka 33 sasa ambapo taifa la Iran limesimama kidete mkabala na njama za maadui na hakuna wakati ambao maadui waliweza kulikwamisha taifa hili katika masuala mbaliambali.

MISRI YATAKA KUIMARISHA UHUSIANO WAKE NA HIZBUL LAH

Balozi wa Misri nchini Lebanon Ashraf Hamdy amesema nchi yake inataka kujenga uhusiano imara na harakati ya muqawama ya Lebanon Hizbullah. Akizungumza katika mahojiano na gazeti la Lebanon la Daily Star Hamdy amesema huwezi kuzungumzia siasa nchini Lebanon pasina kuwa na uhusiano na Hizbullah. Katika kile kinachoonekana kuwa ni mageuzi makubwa ya sera zinazotafautiana na za utawala wa zamani wa dikteta Hosni Mubarak, balozi wa Misri nchini Lebanon amesisitiza kuwa serikali ya Rais Muhammad Mursi itafuata sera ya kuyanyooshia mkono kwa uzito sawa nchi na mirengo yenye ushawishi katika eneo ikiwemo Hizbullah ili kuweza kuwa na mawasiliano ya karibu na viongozi wa Lebanon. Aidha ameongeza kuwa tayari ameshakutana na viongozi wa idara ya kisiasa ya Hizbullah ili kuweza kufahamiana vizuri zaidi. 
Balozi wa Misri amefafanua kuwa Hizbullah imefanya kazi nzuri ikiwa ni harakati ya muqawama katika kulinda ardhi ya Lebanon na kwamba hatua ya harakati hiyo ya kupambana kuyakomboa maeneo ya nchi hiyo yanayokaliwa kwa mabavu na Israel ni halali na ni ya kisheria. Uhusiano wa Misri ya enzi za Mubarak na Hizbullah uliharibika zaidi mwaka 2008 katika vita vya siku 22 vya Israel dhidi ya Ukanda wa Gaza, wakati Katibu Mkuu wa Hizbullah Sayyid Hassan Nasrullah alipoikosoa Cairo kwa kushindwa kuwasaidia Wapalestina

M23 WASHAMBULIA HELIKOPTA YA UN

Kikosi cha kulinda amani cha Umoja wa Mataifa katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo kimesema kuwa waasi wa harakati ya Machi 23 wamezishambulia helikopta zake mbili huko mashariki mwa Kongo. Ujumbe wa Umoja wa Mataifa Monusco umesema katika taarifa yake ya jana kwamba helikopta mbili za umoja huo zilishambuliwa Jumatano usiku iliyopita katika anga ya miji ya Kibumba na Kanyamahahoro inayodhibitiwa na waasi wa M23.
Taarifa ya Monusco imeongeza kuwa hii ni mara ya pili kwa waasi wa Machi23 kuzishambulia helikopta za Umoja wa Mataifa kwa makusudi na kwamba wale waliohusika watachunguzwa na kufikishwa mbele ya vyombo vya sheria. Hata hivyo Luteni Kanali Vianney Kazarama msemaji wa waasi wa harakati ya M23 amekanusha madai kuhusu kushambuliwa helikopta hizo za Umoja wa Mataifa.

NIGERIA WAENDA KULINDA AMANI SOMALIA

Serikali ya Nigeria imetangaza kuwa hivi karibuni itatuma wanajeshi 140 nchini  Somalia chini ya mwamvuli wa Kikosi cha Kulinda Amani cha Umoja wa Afrika AMISOM. Kayode Aderanti Afisa Mwandamizi wa Vikosi vya Kulinda Amani katika jeshi la Nigeria amesema kuwa, wanajeshi hao wa Nigeria wanatumwa nchini Somalia kutokana na makubaliano yaliyofikiwa hivi karibuni kati ya serikali ya Abuja na Umoja wa Afrika. Nchi ya Somalia inashuhudia mapigano na machafuko tokea ulipopinduliwa utawala wa Jenerali Muhammad Siad Barre mwaka 1991, kati ya serikali ya mpito na makundi yenye misimamo ya kufurutu mipaka likiwemo al Shabab. Umoja wa Afrika tokea mwaka 2007 uliunda kikosi cha kulinda amani AMISOM kwa shabaha ya kuisaidia serikali ya mpito ya Somalia kukabiliana  na makundi ya waasi nchini humo.

SAIF ISLAM KUFIKISHWA MAHAKAMANI MWEZI UJAO


Mwana wa kiume wa dikteta wa zamani wa Libya Saiful Islam Gaddafi na mkuu wa zamani wa vyombo vya ujasusi vya nchi hiyo Abdullah Sanoussi watafikishwa mahakamani mwezi ujao. Msemaji wa Mwendesha Mashtaka Mkuu wa Libya Taha Bar'a amesema kuwa kesi ya Seiful Islam na Sanoussi itafanyika mwezi ujao mjini Tripoli licha ya wito wa Mahakama ya Kimataifa ya Jinai (ICC) inayotaka ikabidhiwe mwana huyo wa Gaddafi.
Msemaji wa mahakama ya ICC Fadi al Abdullah amesema mahakama hiyo ya kimataifa italichukua faili la kesi ya Saiful Islam Gaddafi iwapo mahakama za Libya hazitasimamia kesi yake kwa uadilifu. Ameongeza kuwa viongozi wa Libya wameahidi kwamba wataheshimu sheria za kimataifa katika uendeshaji wa kesi hiyo. Saiful Islamu Gaddafi anakabiliwa na tuhuma za kutenda jinai dhidi ya binadamu na jinai za kivita.

Friday, December 28, 2012

MAREKANI KUANZA VIKAO MASUALA YA KIFEDHA


Rais wa Marekani Barack Obama leo ataongoza mkutano wa viongozi wa bunge ikiwa ni pamoja na mahasimu wake wakuu wa chama cha Republican katika jitihada za mwisho za kuizuia Marekani kuelekea katika kile kinachofahamika kama mkwamo wa kiuchumi.
Afisa wa Ikulu ya White House amesema Obama atakutana na mahasimu wake wa Republican Spika wa Baraza la wawakilishi John Boehner na Kiongozi wa upande wa viti vichache katika Seneti Mitch McConnell na washirika wake wa Democratic Kiongozi wa upande wa viti vingi katika Seneti Harry Reid, na Kiongozi wa upande wa viti vichache katika Baraza la Wawakilishi Nancy Pelosi. Mkutano huo unakuja wakati kukiwa na ongezeko la mvutano wa kisiasa na kuongezeka wasiwasi nchini Marekani kuhusu kama muafaka dhabiti utaweza kupatikana kabla ya kumalizika mwaka huu ikiwa ndio muda wa mwisho. Siku ya Jumatano Obama alizungumza na viongozi hao wanne McConnell, Reid, Boehner na Pelosi akitaraji kusonga mbele katika mpango huo lakini wabunge na wasaidizi wao wamesisitiza kwamba hakuna hatua zozote zilizopigwa wakati wa msimu huu wa likizo.

KAMANDA ALIYESAIDIA KUMUONDOA SADDAM HUSSEIN KUWAIT AFARIKI

Norman Schwarzkopf, Jenerali wa Marekani aliyeongoza Operesheni ya kijeshi iliyopewa jina la Uvamizi wa Jangwani, ambayo iliikomboa Kuwait kutoka mikononi mwa kiongozi wa Ki imla wa Iraq Saddam Hussein mnamo mwaka wa 1991, ameaga dunia akiwa na umri wa miaka 78. Schwarzkopf, amefariki mjini Tampa, ambako alistaafu baada ya jukumu lake la mwisho kama Kamanda Mkuu wa Jeshi la Marekani. Rais wa zamani George H W Bush ambaye kwa sasa yuko katika chumba cha wagonjwa mahututi katika jimbo la Texas, amekuwa wa kwanza kutoa taarifa ya kuomboleza kifo cha mtu ambaye yeye alimchagua kuongoza vita ambavyo vilizipa sifa taaluma zao wote wawili. Taarifa hiyo ya Bush imemtaja Schwarzkopf kama mzalendo halisi wa Marekani na mmmoja wa viongozi wakuu wa kijeshi katika kizazi chake. Jeshi la Saddam Hussein lililokuwa na watu milioni moja liliivamia Kuwait mnamo mwaka wa 1990 na kuonekana kutaka kuingia Saudi Arabia, jambo ambalo lingempa zaidi ya asilimia 40 ya hifadhi za mafuta ulimwenguni. Schwarzkopf aliliweka pamoja jeshi la washirika kutoka nchi 32, ambalo liliviondoa vikosi vya Iraq nchini Kuwait katika wiki chache kupitia mashambulizi makali ya kutokea angani na nchi kavu

MUBAARAK ALAZWA TENA HOSPITALI

Maafisa nchini Misri wamesema rais aliyeondolewa madarakani Hosni Mubarak amehamishwa kutoka gerezani ambako anatumikia kifungo cha maisha, na kupelekwa katika hospitali ya kijeshi kupokea matibabu. Mubarak amerudishwa hospitalini baada ya hali yake ya kiafya kuwa mbaya. Wiki iliyopita, rais huyo wa zamani mwenye umri wa miaka 84 alipelekwa katika hospitali hiyo hiyo kufanyiwa vipimo vya matibabu kutokana na ma majeraha aliyopata ya kichwa na mbavu baada ya kuanguka. Mnamo mwezi Juni, Mubarak alilazwa hospitalini kwa mwezi mmoja baada ya kudaiwa kukosa fahamu.

WAFANYAKAZI WAGOMA ISRAEL

Idadi kubwa ya wafanyakazi wa shirika la bima la utawala wa Kizayuni wa Israel wamefanya mgomo kulalamikia ugumu wa kazi, mazingira mabaya ya kazi na kutopandishwa mishahara yao. Redio ya kijeshi ya utawala huo imetangza kuwa, wafanyakazi hao wamefanya mgomo hii leo baada ya kushindikana kufikiwa makubalino kati yao na serikali ya utawala huo bandia. Hadi sasa viongozi wa Israel, wanafanya juhudi za kufanyika mazungumzo na viongozi wa shirika la bima kwa ajili ya kumaliza mgomo huo. Kabla ya hapo wafanyakazi hao walifanya mgomo kulalamikia kiwango duni cha mshahara walichosema hakilingani na kazi wanazozifanya, mgomo ambao pia ulijiri baada ya kushindikana kupatikana mwafaka kati yao na Wizara ya Fedha ya Utawala huo wa Kizayuni. Ni vyema kuashiria hapa kuwa, utawala katili wa Kizayuni hivi sasa unakabiliwa na hali ngumu ya kiuchumi ambayo imeufanya ushindwe kumaliza vilio vya wafanyakazi wake. Ni hivi karibuni tu utawala huo pia ulishuhudia mgomo wa wauguzi wapatao elfu 28 uliosababisha kusitishwa shughuli za operesheni za upasuaji katika hospitali zake zipatazo elfu 10.

NJIA KUMI ZA KUHIFADHI QUR 'AN. Part 4.


4. HATUA YA NNE
KUCHAGUA WAKATI NA SEHEMU MUNAASIB KWA KUHIFADHI
Kuweka wakati munaasib kwa kuhifadhi ni njia muhimu inayosaidia kuhifadhi. Na wakati wa kuhifadhi inatofautiana kati ya mtu na mtu kuna anayefadhilisha wakati wa Alfajiri au wakati wa Sahar (kabla ya alfajiri) au baada ya Maghrib. Inapasa uchunge yafuatayo:


 1. Kupangilia muda maalum mfano saa moja au masaa mawili muhimu udumu na muda uliojipangia usipunguze.


 2. Kuwa na faragha kamili katika muda uliojipangia ukate mahusiano na wengine ushughulike na kuhifadhi tu bila ya kuathiriwa na chochote mfano simu makelele au sauti za juu. 3. Kuchagua sehemu maalum yenye utulivu na isiyokuwa na chenye kukushawiwishi mfano picha, vitabu, majarida na vinginevyo vinavyoathiri.
 
5. HATUA YA TANO
KUPANGILIA MWANZO WA HIFDHI (KUHIFADHI)
 Kusudio je mwanzo wa kuhifadhi utakuwa mwanzo wa Mus-haf (Al-Faatihah na Al-Baqarah) au mwisho wa Mus-haf (An-Naas), na hili linatofautiana kutokana na uwezo wa mtu ikiwa mtu ana uwezo mzuri wa kusoma bora aanze mwanzo na ikiwa yupo mwanzo katika kusoma bora aanze na Surat An-Naas.


 Natija ya wote wawili kwa Uwezo wa Allaah ni kufikia katika kuhifadhi Kitabu cha Allaah, wangapi wameanza na Surah ndogo na wamefanikiwa kufika mwisho.


 
6. HATUA YA SITA
KUWEKA IDADI YA AAYAH
Uwezo wa kuhifadhi ni Kipaji kutoka kwa Allaah na inatofautiana uwezo huu kati ya mtu na mtu kikubwa kinachonasihiwa mwanzo wa kuhifadhi ni kuweka idadi kamili hata kama una uwezo zaidi. Kuna mtu anaweza kuhifadhi katika kikao kimoja ukurasa mzima katika Mus-haf kisha siku ya pili ameshasahau baadhi ya Aayah alizohifadhi na kuna mwengine anahifadhi kila siku Aayah tano hazidishi na inakuwa Hifdhi yake ni yenye nguvu.


 Amepokea Abu ‘Umar Ad-Daaniy katika “Al-Bayaan” kutoka kwa ‘Uthmaan na Ibn Mas’uud na Ubay bin Ka’ab kwamba: “Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wasallam) alikuwa akiwafundisha Aayah kumi hazidishi zingine mpaka wajifundishe yaliyomo na kuifanyia kazi, Anawafundisha Qur-aan na kuifanyia kazi kwa wakati mmoja.”


 Kutoka kwa Abu ‘Abdir-Rahmaan As-Sulamiy anasema: “Tulikuwa tukijifundisha Aayah kumi katika Qur-aan hatuchukui zingine baada yake mpaka tujue halali yake na haramu yake, amri yake na makatazo.” Na katika kuweka idadi ya Aayah ni kutokana na kutofautiana urefu wake. Mfano tuchukulie “Aayatud-Dayn” ambayo ni Aayah ndefu kuliko zote katika hali hii inapendekezwa kuhifadhi Aayah kuendana na idadi ya mistari. Ama ikiwa Aayah ni ndogo ndogo mfano Suratul As-Swaaffaat, ‘Abasa, At-Takwiyr na zinginezo jiwekee Aayah kumi au tano katika kikao kimoja. Na ukisoma Tafsiyr kuhusu maana ya maneno ni jambo litakalokusaidia katika kuhifadhi. 


 itaendelea Ijumaa ijayo insha-Allah..............

ASKOFU MKUU WA LEBANON AUKUBALI MPANGO WA IRAN JUU YA SYRIA

Askofu Mkuu wa Lebanon John Maron amekaribisha mpango wenye vipengele sita ulioandaliwa na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, kwa ajili ya kumaliza mgogoro wa kisiasa nchini Syria. Askofu Maron aliyasema hayo leo alipokutana na Balozi wa Iran nchini Lebanon Ghazanfar Rokn Abadi na kusema kuwa, mpango huo wenye vipengee sita kwa ajili ya kumaliza mgogoro wa Syria, ni hatua muhimu kwa ajili ya nchi hiyo na eneo zima kwa ujumla. Kwa upande wake Balozi Ghazanfar, ametoa pongezi kwa mnasaba wa sherehe za kuadhimisha kuzaliwa Nabii Issa (as) na kusema kuwa, Syria itakuwa mhimili mkubwa wa kuimarisha usalama na uthabiti wa eneo ikiwemo Lebanon. Mpango huo wa amani ulioandaliwa na Iran, ulianza kusambazwa hivi karibuni na Wizara ya Mambo ya Nje kwa pande mbalimbali husika nchini Syria na eneo zima la Mashariki ya Kati kwa ujumla.  

WAASI WA MALI WATISHIA KUWAUWA VIONGOZI WA DINI

Viongozi wengi wa dini ya Kiislamu nchini Mali, wamepatwa na wasi wasi kufuatia vitisho vilivyotolewa na makundi ya waasi wa kaskazini mwa nchi hiyo dhidi yao. Duru za habari zinaarifu kuwa, viongozi wengi wa Kiislamu akiwemo sheikh Chérif Ousmane Madani Haïdara mmoja wa masheikh mashuhuri wa nchini Mali, wanakhofia maisha yao kufuatia vitisho hivyo. Leo sheikh Ousmane amenukuliwa akisema kuwa, siku kadhaa zilizopita alipata vitisho vya moja kwa moja au visivyo moja kwa moja kupitia jamaa zake wa karibu, akitishiwa maisha yake kutoka kwa makundi ya kigaidi nchini humo. Kiongozi huyo wa kidini ambaye anaongoza taasisi moja ya kidini yenye wafuasi wengi wa Kiislamu amelieleza shirika la habari la Kifaransa kuwa, Waislamu wa Mali wanapinga vitendo na mienendo ya makundi hayo ya kigaidi na kwamba, vitendo vya kigaidi vinapingwa na dini tukufu ya Kiislamu. Baada ya mapinduzi ya kijeshi yaliyojiri mnamo tarehe 22 Machi nchini Mali, makundi ya Tuareg na Ansarud-Din, yalilishikilia eneo la kaskazini mwa nchi hiyo na kuanzisha oparesheni za kuharibu turathi za Kiislamu nchini humo.

MAANDAMANO MAKUBWA YAFANYIKA RIYADH, SAUDI ARABIA


Kupanuka wimbi la maandamano katika maeneo tofauti ya Saudi Arabia ukiwemo mji mkuu wa Riyadha, kumepelekea kuongezeka mashinikizo kwa utawala wa ukoo wa Aal Saud kwa ajili ya kufanyika marekebisho katika siasa za utawala huo. Katika siku za Jumatatu na Jumanne, umati mkubwa wa Wasaudia ulifanya maandamano katika maeneo tofauti ya nchi hiyo, ukiwemo mji mkuu Riyadh, wakitangaza mfungamano wao na wafungwa wa kisiasa wanaoendelea kushikiliwa katika jela za utawala huo na kutaka kukomeshwa adhabu dhidi ya wafungwa hao. Waandamanaji pia walizitaka taasisi na asasi mbalimbali za haki za binaadamu nchini humo na zile za kimataifa, kufichua jinai zinazotendwa na utawala wa Aal Saud dhidi ya wafungwa wa kisiasa, sambamba na kuwashinikiza viongozi wa utawala huo wawaachie huru wafungwa hao ambao kwa muda mrefu wamekuwa wakishikiliwa katika jela bila ya kufikishwa mahakamani.
Sambamba na kupanuka kwa mwamko wa Kiislamu Mashariki ya Kati na Kaskazini mwa Afrika, wananchi wa Saudia pia walianzisha maandamano ya amani, wakitaka kufanyika marekebisho ya kisiasa na kiuchumi nchini humo. Mfalme mgonjwa wa Saudia ambaye alishuhudia mwisho mbaya wa madikteta wenzake huko Tunisia na Misri, alifanya njama ya kuwahonga wananchi wa nchi hiyo kwa kuwapa fedha ili waachane na maandamano dhidi ya utawala wake. Hata hivyo juhudi hizo hazikumsaidia mfalme Abdullah wa Saudia kwani maandamano katika maeneo ya mashariki yamezidi kupanuka na kufika katika maeneo na sekta nyingine vikiwemo vyuo vikuu. Aidha katika kulalamikia ukosefu wa usawa na kufumbiwa macho haki zao nchini humo wanawake nao wamemiminika mabarabarani na kuendesha magari kwa lengo la kudhihirisha uasi wao wa kiraia kwa utawala wa nchi hiyo. Utawala wa Saudi Arabia ambao umefananishwa na taasisi za haki za binaadamu kuwa sawa na ngome ya udikteta, unaendeleza vitendo vya ukandamizaji, kamatakamata, adhabu kali na kuwazuilia kwa muda mrefu katika jela zake wapinzani na wanaharakati wa kisiasa nchini. Ukandamizaji huo unaofanywa na utawala wa Riyadh, umesababisha kuongezeka kwa upinzani nchini humo na kufanya upinzani uliokuwa katika maeneo ya mpakani kuingia katika miji mingine ukiwemo mji mkuu Riyadh.
Kupanuka kwa wimbi la upinzani mjini Riyadh kunaashiria kwamba, wapinzani nchini Saudia, si tu kwamba wanalalamikia huduma za chakula na kiuchumi, bali pia wanapinga udikteta, ukatili na vitendo vinavyokinzana na haki za binaadamu nchini humo. Utawala wa Riyadh unafuata mfumo wa kifalme, ambao unaweka madaraka yote muhimu ya nchi mikononi mwa ukoo wa Aal Saud. Ubaguzi huo wa kisiasa umepelekea kuongezeka ufisadi wa kisiasa na kiuchumi katika muundo wa kisiasa wa Saudia. Utawala wa nchi hiyo umefikia kiwango cha kufumbia macho haki muhimu za raia wake, ukiwemo ushiriki wa kisiasa na haki za kijamii kama vile za uendeshaji magari na upigaji kura kwa wanawake. Mbali na hayo, mfumo wa mahakama wa nchi hiyo unawakandamiza moja kwa moja wapinzani. Karibu wafungwa wa kisiasa elfu 30 wanashikiwa kwa muda mrefu katika jela za Saudi Arabia bila kusomewa mashtaka mahakamani, na wala jamaa zao hawana habari yoyote kuhusiana na mustakbali wao. Na Sudi Jafar

Thursday, December 27, 2012

MZEE MANDELA ARUHUSIWA KURUDI NYUMBANI


Aliyekuwa rais wa Afrika Kusini Nelson Mandela, ameruhusiwa kwenda nyumbani kutoka hospitali moja mjini Pretoria.Ikulu ya rais nchini humo imesema rais huyo wa zamani wa Afrika kusini, anaendelea kupata nafuu nyumbani mwake. Msemaji wa serikali amesema Mandela bado hajapoa kabisa na ataendelea kupokea matibabu nyumbani mwake mjini Johannesburg.
Mandela alilazwa hospitaini siku kumi na nane zilizopita kufuatia maambukizi ya mapafu Mkewe Graca Machel, na rais Jacob Zuma walimtembelea Bwana Mandela siku ya Krismasi na walisema kuwa alikuwa katika hali nzuri. Baada ya ziara hiyo, rais Zuma alisema kuwa madaktari wamefurahishwa na jinsi Bwana Mandela alivyokuwa akiendelea kupona kwa hara licha ya umri wake.
Rais Zuma aliwashukuru raia wa nchi hiyo kwa risala zao za heri njema kwa rais huyo wa zamani. Hata hivyo aliomba raia na waandishi wa haabri kuwa na subira na wakati huo huo kuwapa bwana mandela na familia yake nafasi wanayohitaji.
Hi ni mara ya kwanza tangu mwaka wa 1990 ambapo rais Mandela amelazwa hospitalini kwa muda mrefu zaidi. Mjukuu wa Bwana Mandela, Mandla, amesema, kutokuwepo kwa babu yao wakati wa Krismasi kumewasikitisha sana kwa sababu hawakudhani kuwa angesalia hospitalini kwa muda huo wote.

BARIDI YAUWA WATU 128 RUSSIA


Watu wasiopungua 128 wamekufa kutokana na baridi isiyo ya kawaida nchini Urusi, ambayo imefika nyuzi 30 chini ya sufuri katika kipimo cha Celsius. Shirika la habari la Urusi, Interfax, limesema kuwa watu wengine takriban 900 wamepatiwa matibabu hospitalini kutokana na matatizo yaliyo na uhusiano na baridi. Wengi wa walioathirika ni wale wasio na makazi.
Huku hali hiyo ikijiri nchini Urusi, huko Marekani kimbunga kinachoambatana na barafu kutoka ghuba ya Mexico kimeipiga kanda ya maziwa makuu ya Marekani na kusababisha vifo vya watu saba na kukwamisha usafiri wa anga. Kitengo cha hali ya hewa nchi humo kimeonya kwamba uzito wa barafu unaweza kuangusha miti na miundombinu ya umeme. Tayari watu wapatao laki mbili hawana huduma ya umeme, na maelfu ya watalii wamekwama katika maeneo mbalimbali ya Marekani.

ISRAEL YARUHUSU MALORI YA BIDHAA KUINGIA GAZA


Israel imelegeza vikwazo juu ya bidhaa zinazoingizwa katika Ukanda wa Gaza. Hatua hiyo itaruhusu malori 20 yaliyojaza bidhaa za ujenzi kuingia katika ukanda huo kila siku, hii ikiwa ni mara ya kwanza tangu mwaka 2007.
Radio ya Israel imesema kwamba bidhaa hizo zitaanza kuingia wiki ijayo. Tangazo la radio hiyo pia limesema kwamba Israel imeruhusu kuingizwa kwa mabasi mapya 40 na malori 20 kwa matumizi ya kila siku katika ukanda wa Gaza. Uamuzi wa kuruhusu kuingizwa kwa vifaa vya ujenzi unaonekana kuwa sehemu ya makubaliano yasiyo rasmi, ambayo yalifikiwa baina ya Israel na chama cha Hamas chini ya usuluhishi wa Misri, na ambayo yalisimamisha mapigano makali yaliyoibuka mwezi Novemba mwaka huu kati ya Israel na Hamas.
Vikwazo vya Israel dhidi ya uingizwaji wa bidhaa za ujenzi ndani ya Ukanda wa Gaza viliimarishwa mwaka 2006, kufuatia mfululizo wa mashambulizi ya maroketi kutoka katika ukanda huo na kutekwa kwa mwanajeshi wake.

WASYRIA WALIOUWAWA WAFIKIA 45,000


Idadi ya waliouawa katika vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini Syria ni zaidi ya watu 45,000, hii ikiwa ni kwa mujibu wa shirika la kuchunguza haki za binadamu nchini Syria lenye makao yake nchini Uingereza. Idadi hiyo imetangazwa huku mpatanishi wa kimataifa kuhusu mzozo huo, Lakhdar Brahimi, akielekeza matumaini yake kwa Urusi, kusaidia kutafuta suluhu la amani.
Mkuu wa shirika hilo la kuchunguza haki za binadamu nchini Syria, Rami Abdel Rahman, amesema kuwa watu zaidi ya 1,000 wameuawa mnamo wiki moja iliyopita. Tangazo hilo limezidisha hofu iliyoelezwa na Umoja wa Mataifa kwamba hali ya kibinaadamu inazidi kuwa mbaya nchini Syria. Mjumbe maalumu wa umoja huo kuhusu Syria Paulo Pinheiro amesema ripoti za hivi karibuni zimedhihirisha ghasia zenye misingi ya kikabila.
Wizara ya mambo ya nchi za nje ya Uturuki imesema kwamba Wasyria zaidi ya 1,000 walikimbilia nchini humo katika muda ma saa 24 zilizopita. Wakati huo huo, Marekani imekaribisha kwa tahadhari, taarifa kwamba mkuu wa polisi jeshini General Abdel Aziz Jassem al-Shallal amejitenga na serikali ya Rais Bashar al-Assad na kujiunga na upinzani.

WANAJESHI WA ISRAEL WAJIUA WENYEWE


Wanajeshi wasiopungua 237 wa utawala haramu wa Israel wamejiua katika nyakati mbali mbali katika kipindi cha miaka kumi iliyopita. Kwa mujibu wa nyaraka za siri za jeshi la Israel, kwa uchache wanajeshi 24 wa utawala huo hujiua kila mwaka.
Press TV imesema nyaraka hizo za siri zilitolewa kwa mara ya kwanza na mwanablogi wa Israel ambaye alikamatwa na polisi na kusailiwa. Mwanablogu huyo amesema idadi ya askari wa Jeshi la Israel waliojiua ni zaidi ya iliyotangazwa rasmi. Hivi karibuni Wizara ya Vita ya Israel ilikiri kuwa idadi ya wanajeshi wake wanaojiua ni zaidi ya wanaouawa vitani.
Jeshi la utawala haramu wa Israel limeshindwa kwa madhila mara kadhaa katika vita dhidi ya wanamapambano wa Palestina na Lebanon. Katika hujuma yake ya hivi karibuni dhidi ya Ukanda wa Ghaza, utawala haramu wa Israel ulilazimika kuomba usitishwaji vita baada ya jeshi lake kushindw akukabiliana na maroketi ya wapigania ukombozi wa Palestina.

MTAZAMO WA MAREKANI JUU YA DEMOKRASIA


Uungaji mkono mkubwa wa wananchi wa Misri kwa rasimu ya katiba mpya ya nchi hiyo umeiweka njia panda Marekani ya kuyakubali au kuyakataa matakwa ya kidemokrasia ya Wamisri waliowengi.  Katika radiamali yake ya kwanza kwa asilimia 64 ya kura za wananchi wa Misri walioipigia kura ya ‘ndiyo’ rasimu ya katiba mpya, Washington imetangaza kuwa demokrasia ni zaidi ya matakwa ya kura za waliowengi. Kwa maneno mengine ni kwamba ikiwa katika nchi yoyote ile wananchi waliowengi watalipigia kura za ‘ndiyo’ suala lisiloiridhisha Marekani demokrasia haitokuwa imefikiwa.
Bila ya shaka kuyapuuza matokeo ya kura zinazoakisi matakwa ya wananchi si kitu kigeni na cha ajabu kwa Marekani, na tukio la kura ya maoni ya katiba mpya ya Misri si la kwanza na wala halitokuwa la mwisho. Miaka sio mingi iliyopita wakati wananchi wa Palestina walipoichagua harakati ya Hamas katika uchaguzi wa kwanza huru, Waziri wa Mambo ya Nje wa wakati huo wa Marekani Condoleeza Rice alitamka kwamba demokrasia, haina maana tu ya kulipa uhalali wa kisheria kila kundi linalochaguliwa kwa masanduku ya kura. Ni kwa mantiki hiyo Marekani na Israel zilizidisha mashinikizo kwa wananchi wa Palestina ya kuwakomoa na kuwadhibu kwa sababu tu ya kushiriki katika uchaguzi huru na wa kidemokrasia. Mzingiro wa kiuchumi dhidi ya Gaza na baadaye vita vya siku 22 dhidi ya watu wa eneo hilo zilikuwa miongoni mwa radiamali za Washington na Tel Aviv kwa uamuzi uliochukuliwa na wananchi wa Palestina katika uchaguzi wao wa bunge.
Hivi sasa Marekani inakabiliwa tena na mazingira yanayofanana na yale. Itakumbukwa kuwa kwa miongo kadhaa sasa Washington imekuwa ikijigamba kuwa ndio kiranja na kinara wa uhuru na demokrasia duniani. Lakini licha ya majigambo hayo kuna vielelezo na mifano hai kadha wa kadha inayosuta madai hayo ya Washington. Kwa mfano hakuna asiyejua kuwa katika kipindi chote hiki cha nusu karne iliyopita kumekuwepo na tawala kadhaa za kidikteta na kandamizi zaidi duniani ambazo zilikuwa ni waitifaki wakubwa wa Marekani. Katika baadhi ya nchi Marekani imehusika waziwazi katika mapinduzi ya kijeshi ya kuziangusha serikali halali na zilizochaguliwa na wananchi au kuwasha moto wa vita vya ndani au vya kieneo dhidi ya serikali zisizokubali kuburuzwa na nchi hiyo. Mifano ya aina hii ni mingi mno hususan katika eneo hili la Mashariki ya Kati. Si siri kwamba vuguvugu la mapambano ya wananchi wa eneo hili ambalo vyombo vya habari vya Magharibi vimelipa jina la ‘Msimu wa Machipuo ya Kiarabu’ yalikuwa ni mapambano dhidi ya tawala vikaragosi na vibaraka wa Marekani. Kwani watawala waliong’olewa madarakani kwa mapambano ya wananchi katika nchi za Tunisia na Misri, kwa miongo kadhaa walikuwa wakipata himaya na uungaji mkono wa kiuchumi na kisiasa wa Marekani na nchi za Ulaya licha ya kufanya ukandamizi na ukiukaji mkubwa wa haki za binadamu dhidi ya raia wao. Lakini kwa vile walikuwa wakikidhi na kudhamini maslahi ya Washington waliendelea kupata himaya ya madola ya Magharibi. Kwa kuzingatia rekodi hiyo haitokuwa ajabu ikiwa serikali ya Marekani itatia ulimi puani na kuyakataa matokeo ya kura ya maoni ya katiba ya Misri na kuielezea demokrasia kuwa ni kitu zaidi ya kura na matakwa ya waliowengi. Japokuwa wakati wa harakati za kumng’oa madarakani dikteta Hosni Mubarak na katika matukio yaliyojiri baadaye nchini Misri Washington haikujionyesha waziwazi kuwa iko dhidi ya wananchi wa nchi hiyo lakini kuongezeka harakati za Kiislamu, hisia za kutaka kujitawala na chuki dhidi ya Israel ndani ya Misri kumeitia hofu na wasiwasi mkubwa Marekani. Kwa hivyo tusije tukashangaa kuona serikali iliyochaguliwa kwa ridhaa ya wananchi waliowengi wa Misri na maamuzi yatakayochukuliwa na serikali hiyo, mwishowe yanagongana na kukinzana na maslahi ya Marekani. Endapo hilo litajiri Washington inaweza kuchukua hatua sawa na zile za mwaka 1953 nchini Iran za kuiangusha kupitia mapinduzi ya kijeshi serikali halali ya Waziri Mkuu Dakta Muhammad Musaddiq, mwaka 1973 nchini Chile za kuiangusha kwa mbinu hiyo hiyo serikali halali ya Salvador Allende au za mwaka 2006 za kuiwekea vikwazo ya serikali halali ya Palestina. Kwa maneno mengine ni kuwa Washington ima itaandaa mazingira ya kufanyika mapinduzi ya kijeshi nchini Misri au itaiwekea mbinyo na mashinikizo serikali ili kuwakomoa na kuwatia adabu wananchi wa nchi hiyo. Na sababu ya yote hayo ni kwamba kwa mtazamo wa Marekani demokrasia hukubalika na kutambuliwa rasmi pale tu matokeo yake yanapokidhi na kudhamini maslahi ya nchi hiyo.

MAREKANI INA IDADI KUBWA YA WATOTO WAISHIO BILA BABA


Imebainika kuwa takribani watoto milioni 15 nchini Marekani wanaishi bila baba zao hii ikiwa ni mtoto moja katika kila watoto watatu nchini humo.
Kwa mujibu wa  ripoti ya Idara ya Takwimu Marekani, tatizo la kutoweka baba katika familia linaonekana zaidi katika familia za Wamarekani wenye asili ya Afrika ambapo idadi hiyo ni karibu watoto milioni tano. Wataalamu wa masuala ya jamii wanasema tatizo hilo limepelekea kuongezeka umasikini, uhalifu na utumizi wa madawa ya kulevya Marekani.
Vincent DiCaro Mkuu wa Jumuiya ya Kitaifa ya Kinababa anasema matatizo mengi ya Marekani yanaweza kutatuliwa iwapo wazazi wote wawili wataishi pamoja. Kwa mujibu wa uchunguzi wanandoa wanaoishi pamoja Marekani huwa na pato la takribani dola thamanini elfu kwa mwaka huku akina mama waishio bila waume zao wakiwa na pato la takribani dola 24 elfu kwa mwaka.

WAANDAMANAJI WAFUNGA KITUO CHA MAFUTA


Waandamanaji nchini Libya wamesababisha kufunguwa kituo kikubwa cha kuhifadhi mafuta ghafi ya petroli mashariki mwa nchi hiyo. Naibu Waziri wa Mafuta Libya Omar Shakmak amesema wasimamizi wa Bandari na Kituo cha Mafuta cha Zueitina wameamua  kufunga kituo hicho kwa kuhofia hujuma ya waandamanaji. 'Waandamanaji wanataka serikali iwape nafasi za kazi na wanaamini kuwa wanaweza kuishinikiza serikali kwa kusimamisha shughuli za mashirika  ya uchimbaji mafuta ya petroli', amesema naibu waziri wa mafuta Libya Bandari ya Zueitina husafirisha nje karibu mapipa 60,000 ya mafuta ghafi kila mwaka.
Kwa ujumla Libya husafirisha nje mapipa milioni moja laki sita ya mafuta ghafi kila siku. Tatizo na ukosefu wa ajira ni kati ya changamoto kubwa za viongozi wa Libya ambao wamechukua madaraka nchini humo baada ya kutimuliwa madarakani Muammar Gaddafi aliyeuawa katika mapinduzi ya wananchi yaliyojiri nchini humo mwaka jana.

NETANYAHU ATUMIA PROPAGANDA DHIDI YA IRAN KATIKA KAMPENI ZAKE


Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu na Avigdor Lieberman Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Utawala huo, aliyetangaza kujiuzulu hivi karibuni kufuatia tuhuma za uhaini, kwa pamoja hapo jana walianzisha rasmi kampeni zao za uchaguzi katika ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu.
Katika sherehe za ufunguzi wa kampeni hizo za muungano wa chama cha Likud na Beitenu, Netanyahu alizungumzia changamoto kubwa mbalimbali zinazoikabili Israel, sambamba na kuashiria kadhia ya nyuklia yenye malengo ya amani ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. Netanyahu pia aligusia maudhui nyingine ukiwemo uwezo wa kijeshi wa Harakati ya Hizbullah ya Lebanon na Hamas ya Palestina, kadhia ya kuanguka madikteta katika eneo Mashariki na Kati ya kaskazini mwa Afrika, taathira ambayo imesababishwa na mabadiliko ya kisiasa katika eneo hilo na mporomoko wa uhusiano wa baadhi ya watawala wa Kiarabu na Israel. Aidha ameutaja mwako wa Kiislamu kuwa chanzo cha kuenea kwa Uislamu wa kupindukia mipaka katika Mashariki ya Kati na kuongeza kuwa, baadhi ya watu wanasema kuwa, katika kukabiliana na wimbi hili lazima kusalimu amri na kuinua juu bendera ya amani lakini kwamba Israel haitafanya hivyo chini ya uongozi wake.
Katika miezi ya hivi karibuni Waziri Mkuu huyo wa Utawala haramu wa Israel amefanya juhudi kubwa za kuimarisha nafasi yake iliyodhoofika. Lengo la hotuba yake hiyo, ni kujaribu kuvutia kura na kuzidisha nafasi ya ushindi wa chama cha mrengo wa kulia katika uchaguzi unaotarajiwa kufanyika tarehe 22 Januari mwakani. Ni katika hali hiyo ndio maana kiongozi huyo akafanya njama za ziada za kueneza uvumi na uongo dhidi ya miradi ya kuzalisha nishati ya  nyuklia nchini Iran.
Mfumo huo wa kampeni za Israel unashabihiana sana na stratijia zilizotumiwa na wagombea urais katika kampeni za uchaguzi wa hivi karibuni nchini Marekani, kuhusiana na maudhui ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. Itakumbukwa kuwa katika kikao cha hivi karibuni cha Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, Waziri Mkuu huyo wa Utawala wa Kizayuni wa Israel pia aliwasilisha mchoro wa bomu kwa ajili ya kuonyesha kuwa shughuli za nyuklia za Iran ni tishio kwa usalama wa dunia. Hata hivyo njama hiyo haikuungwa mkono na wajumbe wa baraza hilo na badala yake waziri mkuu huyo akaonekana kama mcheza  tamthilia katika siasa za kimataifa.
Aidha hivi karibuni pia akiwa mbele ya Wazayuni katika hafla ya kumbukumbu ya kuuawa Waziri Mkuu wa zamani wa Israel Ishaq Rabin, Netanyahu alidai kuwa, kwa miaka kadhaa shughuli za nyuklia za Iran zimekuwa zikifanyika kwa malengo ya kijeshi huku ikiendelea kuyafadhili makundi aliyoyataja kuwa ya kigaidi nchini Lebanon na huko katika Ukanda wa Gaza.
Wakati kiongozi huyo mwenye misimamo mikali wa utawala katili wa Kizayuni akizizungumzia shughuli za nyuklia za Iran zenye malengo ya amani, fikra za walimwengu zinauona utawala huo wa Israel kuwa ndio tishio kubwa kwa usalama wa dunia, kutokana na kumiliki kwa uchache vichwa vya silaha za atomiki mia tatu 300 katika vituo vyake vya nyuklia.

MAREKANI KUTUMA MAJESHI NA MAJASUSI AFRIKA


Utawala wa Marekani umetangaza mpango wa kutuma majasusi barani Afrika baada ya kuidhinisha mpango mwingine wa kutuma wanajeshi 4,000 katika nchi 35 za bara hilo. Imearifiwa kuwa Wakala wa Kijasusi katika Jeshi la Marekani DIA imeshaanza kutuma majasusi wa kijeshi katika maeneo mbali mbali ya Afrika.
Hatua hiyo inaashiria kuwa Marekani ina njama kubwa zaidi kuliko inavyodai kuwa lengo lake ni kutoa mafunzo kwa wanajeshi katika nchi za Afrika. Marekani imeimarisha mikakati yake ya kijeshi barani Afrika baada ya kushuhudiwa mwamko mkubwa wa Kiislamu katika nchi za Afrika Kaskazini. Mwamko huo wa Kiislamu umepelekea kutimuliwa madarakani madikteta waliokuwa vibaraka wa Marekani huko Tunisia, Misri na Libya. Hivi karibuni serikali ya Marekani ilisema inakusudia kutuma majeshi yake katika nchi 35 za Kiafrika kwa kisingizo cha kukabiliana na tishio la vitendo vya kigaidi barani humo. Wanajeshi hao wa Marekani watatumwa katika nchi za Afrika Mashariki kama vile Kenya na Uganda.

JUMLA YA WATOTO 41 WALIUWAWA KWA MASHAMBULIO YA ISRAEL DHIDI YA HAMAS

Shirika la kimataifa la kutetea haki za binaadmau Amnesty International limethibitisha kwamba watoto 41 wa Kipalestina waliuawa katika mashambulizi ya siku 8 yaliyofanywa na majeshi ya utawala wa Israel katika eneo la Ukanda wa Gaza. Taarifa iliyotolewa leo na shirika hilo imeeleza kuwa, maafa yaliyosababishwa na majeshi ya Israel katika kipindi cha siku 8 ni makubwa zaidi kuliko mashambulizi yaliyofanyika mwishoni mwa mwaka 2008 huko Gaza. Amnesty International imeeleza kuwa, mauaji dhidi ya watoto katika vita vya utumiaji silaha, yanahesabiwa kuwa jinai kubwa dhidi ya binadamu. Amnesty International imezitaka kamati maalumu za Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa na asasi nyingine za kimataifa kuendeleza uchunguzi wao kuhusiana na mashambulizi ya Israel dhidi ya raia wa Palestina wa eneo la Gaza. Serikali ya Palestina iliyochaguliwa na wananchi na inayoongozwa na Hamas imeeleza kuwa, mashambulizi ya siku 8 huko Gaza yalipelekea watu 185 kuuawa shahidi na wengine 1,399 kujeruhiwa.

SOMALI YAWATAKA AL SHABAAB KUWEKA SILAHA CHINI


Somalia imewapa muda wa siku 120 wapiganaji wa as Shabab ili waweke silaha zao chini na kujiunga na mpango wa amani na kujenga taifa. Abdikarim Guled Waziri wa Mambo ya Ndani na Usalama wa Taifa wa Somalia amesema kuwa, serikali pia imewataka vijana wanaopigana katika kundi hilo wajisalimishe na kuondoka kwenye kundi hilo.
Aidha amewataka wapiganaji wa as Shabab kuacha fikra za kuzusha machafuko na vita, na kuahidi kuwa serikali itawasamehe vijana watakaojisalimisha, kwani wamelaghaiwa na kutiwa kasumba.
Taarifa zinasema kuwa, wafuasi wasiopungua 550 wa kundi la as Shabab hadi sasa wamelikimbia kundi hilo na kujisalimisha kwa maafisa wa serikali ya Somalia. Kundi hilo mwaka 2006 lilijitoa katika Muungano wa Mahakama za Kiislamu (UIC) na kuanza harakati na mapigano kwa lengo la kuangusha serikali ya mpito ya Somalia.

Wednesday, December 26, 2012

WANAWAKE MRUFUKU KUVAA NGUO FUPI


Wanawake nchini Swaziland wako katika hatari ya kukamatwa na polisi iwapo watavaa sketi fupi au blauzi ambazo zitaonyesha tumbo likiwa wazi. Msemaji wa polisi Wendy Hleta amesema polisi watatekeleza sheria ya mwaka1889 ambayo inapiga marufuku uvaaji wa nguo zinazokosa maadili.
Hata hivyo, sheria hiyo ya kikoloni haitumiki katika uvaaji wa nguo za kijadi ambazo zinavaliwa na wanawake, sehemu kubwa ya miili yao inaachwa wazi.Msemaji huyo wa polisi pia amesema wanawake wanaovaa nguo fupi ni kivutio cha wabakaji. Mavazi hayo huvaliwa wakati wa sherehe, zikiwemo za mwaka zinazompa Mfalme fursa ya kuchagua mke wake mpya.Mwaka 2000, serikali ilitunga sheria inayowataka wanafunzi wa kike kuanzia miaka 10 na zaidi kuvaa sketi zinazovuka magoti kama njia ya kuwalinda dhidi ya maambukizi ya Ukimwi.

Swaziland ina idadi ya watu milioni1.2 na moja kati ya nchi zenye kiwango kikubwa cha maambukizi ya ukimwi duniani. Bi Hleta amesema sheria hiyo ya mwaka 1889 haijaweza kutekelezwa katika miaka ya karibuni.Amesema polisi wanataka kuwajulisha wanawake kuwa sheria hiyo bado ipo na inafanya kazi. Baadhi ya wanaume katika mji wa Manzini wamesemekana kuwalalamikia wanawake wanaovaa kuvaa nguo fupi.

MRIPUKO MKUBWA WATOKEA NIGERIA


Moto mkubwa umetokea katika mji mkuu wa Nigeria Lagos.
Taarifa zinaarifu kuwa moto huo ulianza katika eneo la kuhifadhi baruti na kisha kuenea kwa haraka katika majengo mengine yaliyo karibu na ghala hilo. Moshi mkubwa umeenea kote katika kisiwa cha Lagos na wazima moto wanajithidi kuuzima moto huo. Bado baadhi yamajengo yanaendelea kuteketea.
Mwandishi wa BBC anasema maafisa wa kuzima moto walikuwa na wakati mgumu kufika eneo hilo kutokana na idadi kubwa ya watu waliokuwa hapa. Kwingineko, maafisa wa usalama Kaskazini mwa Nigeria wanasema watu waliojihami kwa bunduki wamefyetua risasi na kuwaua watu sita katika kijiji chenye idadi kubwa ya wakristo. Msemaji wa jeshi ameiambia BBC, kuwa washambuliaji hao waliwafyetua risasi waumini katika kanisa dogo wakati wa ibada ya Krismasi. Mshambuliaji mmoja amezuiliwa na maafisa wa usalama katika eneo hilo. Ripoti zaidi zinasema kuwa ulinzi umeimarishwa ili kuwaondoshea wasiwasi wakaazi wa eneo hilo.
Hakuna kundi lililodai kuhusika na shambulio hilo katika jimbo la Yobe, lakini kundi lenye itikadi kali za dini ya Kiislamu la Boko Haram limekuwa likiwalenga Wakristo katika eneo hilo mara kwa mara.

WAMAREKANI WASHAMBULIWA TENA AFGHANISTAN

Bomu la kutegwa garini limelipuka karibu na kambi ya kijeshi ya Marekani mashariki mwa Afghanistan na kupelekea watu wasiopungua watatu kuuawa na wengine 7 kujeruhiwa. Sediq Sediqqi Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Afghanistan amesema kuwa, mlipuko huo umetokea katika lango la Kambi ya Chapman ya Marekani kwenye mji wa Khost nchini humo. Kundi la Taliban limetangaza kuhusika na shambulizi hilo ambapo msemaji wa kundi hilo Zabihullah Mujahid amesema, limefanywa ili kuwalenga wale wanaowahudumia Wamarekani katika kambi hiyo. Mlipuko huo umetokea siku moja baada ya polisi mmoja wa kike wa Kiafghani kumuua mshauri wa polisi ya Marekani katika makao makuu ya polisi mjini Kabul. 

MAANDALIZI YA KUKUSANYA SILAHA YAANZA LIBYA

Wizara ya Mambo ya Ndani ya Libya imetangaza kuwa inatayarsha mpango kwa ajili ya kukusanya silaha haramu na kusambaratisha makundi ya wanamgambo ili kurejesha amani na usalama nchini humo. Majdi al A'rafi msemaji wa wizara hiyo ametangaza kuwa, mpango huo unatayarishwa kwa ushirikiano na mkuu wa vikosi vyote vya jeshi la Libya na kwa uungaji mkono wa taasisi za kiraia, mashekhe, wafanyabiashara tofauti na vyombo vya habari vya nchi hiyo.
 Afisa huyo wa Libya ameongeza kuwa, kuwepo silaha mikononi mwa raia kinyume cha sheria kunakwamisha jitihada za serikali za kutekeleza mipango ya maendeleo, kwani mashirika ya kigeni yaliyokuwa yakijishughulisha na shughuli tofauti za kimaendeleo kabla ya mapinduzi ya Libya zenye thamani ya mabilioni ya dola hivi sasa hayako tayari kurejea nchini humo kutokana na ukosefu wa usalama.

WAPALESTINA WAIONYA TENA ISRAEL JUU YA MAKUBALIANO

Utawala wa Kizayuni wa Israel umeendelea kuvunja makubaliano ya kusimamisha vita huko Ghaza. Makundi ya Palestina likiwemo la HAMAS yametoa onyo kali kwa utawala huo dhalimu na kusisitiza kuwa Israel ndiyo itakayokuja kulaumiwa wakati makubaliano ya kusimamisha vita yatakapovunjika. Musa Abu Marzuq, Naibu wa Mkuu wa Ofisi ya Kisiasa ya Hamas ameonya kuwa itafika wakati makundi ya Palestina yatalazimika kujibu uchokozi wa mara kwa mara wa utawala wa Kizayuni wa Israel na huo ndio utakaokuwa mwisho wa makubaliano ya hivi sasa ya kusimamisha vita. Kwa mujibu wa makubaliano yaliyopelekea kusimamishwa vita vya siku nane vilivyoanzishwa na utawala wa Kizayuni huko Ghaza, Israel iliahidi kuheshimu vipengee vya makubaliano hayo kama vile kuacha chokochoko zake dhidi ya Wapalestina na kufungua vivuko vyote vya kuingia na kutoka Ghaza, hata hivyo hakuna kipengee hata kimoja kilichoheshimiwa na utawala wa Kizayuni. Mwezi uliopita wa Novemba, utawala wa Kizayuni ulilazimika kusimamisha mashambulizi yake huko Ghaza siku nane baada ya kuanzisha mashambulizi hayo kutokana na kukabiliwa na mashambulizi ya mamia ya makombora ya wanamapambano wa Palestina. Takwimu zinaonyesha kuwa Wazayuni walishindwa vibaya kiasi kwamba viongozi kadhaa wa utawala wa Kizayuni wamejiuzulu. Ushahidi mwingine unaoonyesha kuwa Israel haikutarajia kupata majibu makali kutoka kwa Wapalestina ni ile hatua yake ya kufanya haraka kukubali masharti ya Wapalestina katika makubaliano ya kusimamisha vita hivyo. Hata hivyo na kama ilivyotarajiwa, Israel haijaheshimu kabisa vipengee vya makubaliano hayo. Hadi hivi sasa haijafungua vivuko vya kuingia na kutoka Ghaza, inaendelea kuuzingira ukanda huo, inafanya chokochoko za mara kwa mara na vitendo vingine mbalimbali vya kuwachochea Wapalestina. Wachambuzi wa mambo wanaamini kuwa kitendo cha utawala wa Kizayuni cha kutoheshimu makubaliano hayo ni kujaribu kujionyesha kuwa bado una nguvu baada ya kupata fedheha ya kukubali masharti ya watu waliozingirwa kila upande kwa miaka kadhaa licha ya Israel kujidai kuwa ni  moja ya madola yenye jeshi kubwa na kali zaidi duniani. Si hayo tu, lakini pia ripoti zinasema kuwa Israel imeshadidisha mateso yake dhidi ya mateka wa Kipalestina na inaendelea kiujeuri kujenga vitongoji vya walowezi wa Kizayuni, yote hayo ikiwa ni kutaka kujionyesha kuwa ina nguvu za kufanya inalotaka. Hata hivyo weledi wa mambo wanaamini kuwa Israel ya hivi sasa ni dhaifu sana ikilinganishwa na ya miaka ya huko nyuma. Sambamba na hayo, wanamapambano wa Palestina nao wameonya kutoa majibu makali zaidi dhidi ya utawala wa Kizayuni iwapo utaendelea kuvunja makubaliano ya kusimamisha vita, jambo ambalo bila ya shaka linawatia hofu kubwa walowezi wa Kizayuni.

MAMIA YA WATOTO KONGO WAMETENGANA NA WAZAZI WAO


Shirika la Kuwahudumia Watoto la Umoja wa Mataifa (Unicef) limeripoti kuwa mamia kadhaa ya watoto wanaendelea kutengana na kuishi mbali na wazazi wao huko Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo baada ya karibu raia milioni moja kukimbia mapigano ya hivi karibuni huko mashariki mwa nchi hiyo. Unicef imetangaza kuwa jumla ya watoto 776 wakiwemo wa kike 429 walio na umri kati ya miezi sita na miaka kumi na nne wanalelewa na ndugu wa familia mwezi mmoja baada mapigano yaliyojiri kati ya vikosi vya serikali ya Kongo na waasi wa harakati ya M23 kwa ajili ya kuudhibiti mji muhimu wa Goma kuwalazimisha karibu watu milioni kuzikimbia nyumba zao.

MATAMSHI YA MAREKANI JUU YA UGAIDI MZURI NA MBAYA YAKOSOLEWA

Sergei Lavrov Waziri wa Mambo ya Nje wa Russia amesema ugaidi ni ugaidi tu akisisitiza kuwa hatua ya nchi za Magharibi ya kuugawa ugaidi huko Syria katika mafungu mawili yaani ugaidi mzuri na mbaya inatilia shaka madai ya nchi hizo kuhusu demokrasia. Waziri wa Mambo ya Nje wa Russia amesema ni jambo lilisokubalika kwa nchi za Magharibi kuwaunga mkono magaidi huko Syria. Amesema nchi za Magharibi zimeugawa ugaidi katika mafungu mawili yaani ugaidi mzuri na mbaya na kwamba hatua hiyo haikubaliki kabisa. Amesema hivi na hapa ninamnukuu " Iwapo tutafuata mantiki hiyo basi kuna uwezekano ikatutumbukiza katika hali hatari zaidi si tu katika eneo la Mashariki ya Kati, bali katika pembe nyingine za dunia pia," mwisho wa kunukuu. Lavrov amesema si jambo jipya kwa nchi za Magharibi kuamua kuugawa ugaidi katika mafungu mawili. 

MALI YAPINGA KUINGIA MALI KIJESHI

Serikali ya Tunisia imetangaza kuwa, inapinga aina yoyote ya uingiliaji kijeshi nchi za kigeni huko Mali. Hayo yamesemwa na Waziri wa Mambo ya Ndani wa Tunisia Ali al Aridh alipokutana na Waziri mwenzake wa Mambo ya Ndani wa Algeria Dahou Oueld Kablia na kuongeza kuwa, nchi yake inapinga suala hilo kwa kuwa uingiliaji kijeshi katika nchi hiyo ya Afrika, utaharibu zaidi hali ya nchi hiyo. Amesema kuwa, Tunisia ina mitizamo ya pamoja na nchi jirani yake Algeria kuhusiana na mgogoro wa Mali na kwamba, kwa mara kadha zimekuwa zikipinga hatua ya uingiliaji wa madola ya kigeni katika juhudi za kumaliza mgogoro wa nchi hiyo. 
Amesisitiza kwamba, mgogoro wa Mali lazima utatuliwe kwa njia za kisiasa na kiusalama. Jana Waziri wa Mambo ya Ndani wa Algeria aliyekuwa safarini nchini Tunisia, alikutana na kufanya mazungumzo na Waziri Mkuu wa nchi hiyo Hamadi al Jabali. Siku ya Alkhamisi iliyopita, Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa lilipitisha muswada uliopendekezwa na Ufaransa kuhusu uingiliaji kijeshi nchini Mali.